26.3 C
New York

Idi Amin; Utata wa ‘birthday’, usaliti na udikteta wake (8)

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIKA sehemu ya saba, tuliona namna Idi Amin alivyoagiza Wakenya waliokuwa wakiishi Uganda kuuawa, akiamini nchi hiyo jirani iliwasaidia makomandoo wa Israel katika operesheni ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe. Endelea …

Hali hiyo ilisababisha kuyumba kwa uhusiano kati ya Uganda na Kenya. Februari, 1976, Idi Amin aliibua madai kuwa Magaribi mwa Kenya ni sehemu ya ardhi ya Uganda.

Hata hivyo, haikuwa Kenya pekee, Idi Amin alikuwa pia na uhusiano mbaya na Rwanda, akitishia mara kadhaa kuulipua kwa mabomu na kuushambaratisha Mji Mkuu wake, Kigali.

Januari, 1977, Idi Amin alimteua Jenerali alimteua aliyekuwa Jenerali wa jeshi, Mustafa Adrisi, kuwa Makamu wake wa Rais. Mwaka huo, ukaibuka mpasuko jeshini. Upande mmoja ukimsapoti Idi Amin na mwingine ukimuunga mkono Adrisi.

Kwa waliokuwa wakimsapoti Adrisi, ambao wengi wao walikuwa na nyadhifa kubwa serikalini, msimamo wao ulikuwa ni kuondosha wageni, hasa Wasudan, kwenye jeshi lao.

Mpasuko huo ulisababisha majaribio kadhaa ya kupindua Serikali ya Idi Amin. Moja ya jaribio hilo ni lile la Juni, 1977, lililofahamika kwa jina la ‘Operation Mafuta Mingi’, ambapo Idi Amin alijeruhiwa.

Baada ya kuuawa kwa Mchungaji Luwum na mawaziri Oryema na Oboth Ofumbi mwaka 1977, viongozi wenzake wengi walijiuzulu na hata kukimbilia ughaibuni.

Kufikia mwaka 1978, Idi Amin alishapoteza ushawishi hata kwa baadhi ya waliokuwa wakimuunga mkono, hiyo ikitokana na Uganda kukabiliwa na mdororo wa kiuchumi na hali mbaya ya miundombinu.

Mwanzoni mwa mwaka 1978, Adrisi alijeruhiwa katika ajali ya gari na kwenda kutibiwa Cairo, Misri. Ajali hiyo iliibua hasira za wafuasi wake walioamini lilikuwa ni jaribio la kumuua.

Novemba, 1978, wanajeshi waliokuwa wakimuunga mkono Adrisi walianzisha vuguvugu la kumng’oa Idi Amin lakini walizidiwa na vikosi vya Serikali, hivyo kusogea mpakani mwa Uganda na Tanzania.

Wakati mapigano yakiendelea mpakani, wanajeshi wa Uganda chini ya Idi Amin walivuka na kuingia Tanzania kwa sababu ambazo hazikufahamika moja kwa moja.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanasema Idi Amin aliagiza wanajeshi wake kuivamia Tanzania kwa madai kwamba Rais wa wakati huo, Mwalim Julius Nyerere alianzisha vita baada ya kuichukua Kagera katika ardhi ya Uganda.

Januari, 1979, Mwalimu Nyerere aliandaa jeshi kwa vita ya kujibu, akisaidiwa na makundi ya Waganda waliokuwa uhamishoni nchini Tanzania na kuunda Jeshi la Ukombozi la Uganda (Uganda National Liberation Army).

Wakati wa vita hivyo, jeshi la Idi Amin lilisaidiwa na Libya ya Muammar Gaddafi, Palestina na wakati huo huo alisafiri kwenda nchi mbalimbali, zikiwamo Saudi Arabia na Iraq, ili kuomba msaada.

Kipindi hicho, tofauti na miaka yote ya utawala, ilikuwa nadra kumuona hadharani Idi Amin na mara nyingi alisikika akihutubia kupitia vituo vya redio na televisheni.

Baada ya kuonekana amezidiwa kabisa Machi, 1979, baadhi ya wanajeshi wa Uganda walimuomba ajiuzulu lakini Idi Amin aliwajibu kwa hasira akisema: “Kama hamtaki kupigana, nitapigana peke yangu.”

Usikose sehemu ya tisa ya makala haya … Kama umepitwa na sehemu zilizopita, tembelea www.gazetini.co.tz

Related articles

Recent articles