Na mwandishi wetu, Gazetini
TUME ya Madini imetoa muda wa siku 30 kwa wamiliki na wawezeshaji wa miradi ya uchimbaji mdogo yenye Mikataba ya Msaada wa Kiufundi kurekebisha mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi wa miradi 128, huku ikionya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaoshindwa kutekeleza matakwa yaliyowekwa.
Kati ya miradi hiyo, 42 ilibainika kutofanya kazi, huku miradi 86 ikiendelea na shughuli za uchimbaji, lakini ikiwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa shughuli na uzingatiaji wa masharti ya Mikataba ya Msaada wa Kiufundi.
Akizungumza jijini Dodoma leo, Jumatano, Agosti 26, 2026, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amesema Tume imetoa Hati za Makosa zenye muda wa siku 30 kwa wamiliki wa miradi 42 iliyobainika kutofanya kazi, ili wawasilishe mrejesho wa hatua walizochukua kurejesha shughuli za miradi hiyo kwa mujibu wa sheria na masharti ya ridhaa za Msaada wa Kiufundi.
Amesema ukaguzi huo ulifanyika kufuatia maelekezo ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, yaliyotolewa Aprili 27, 2026, wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Kwa mujibu wa Lwamo, ukaguzi umebaini baadhi ya miradi inayofanya kazi kutotekeleza ipasavyo mipango inayotakiwa kisheria, ikiwemo Mpango wa Usimamizi wa Mazingira, Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), Mpango wa Uhawilishaji wa Teknolojia, Mpango wa Uchimbaji na Mpango wa Ufunguaji wa Mgodi.
Amesema wamiliki wa miradi 86 inayofanya kazi, pamoja na wawezeshaji wa Msaada wa Kiufundi, wamepewa siku 30 kurekebisha kasoro hizo kwa mujibu wa Kanuni za Msaada wa Kiufundi kwa Wamiliki wa Leseni Ndogo za Uchimbaji Madini za mwaka 2025.
“Endapo wahusika wa miradi hiyo watashindwa kutekeleza matakwa yaliyowekwa ndani ya muda huo, Tume ya Madini itachukua hatua zaidi za kisheria, ikiwemo kufuta ridhaa za Msaada wa Kiufundi,” amesema Lwamo.
Amesema Tume itaendelea kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara katika miradi inayotekelezwa kupitia Msaada wa Kiufundi ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa kuzingatia Sheria ya Madini, kanuni zake na masharti ya ridhaa zilizotolewa.
Aidha, amewataka wanufaika wa Msaada wa Kiufundi na wachimbaji wadogo kuzingatia utunzaji wa mazingira, usalama na afya mahali pa kazi, hususan katika kipindi hiki cha tahadhari kuhusu uwezekano wa mvua za El Niño.
Amesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Tume ya Madini kuimarisha usimamizi wa uchimbaji mdogo, kuhakikisha Msaada wa Kiufundi unatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa na kuongeza tija, usalama na uendelevu wa sekta ya madini nchini.


