29.1 C
New York

Mlima wa Iran unaoipasua kichwa Marekani

Published:

TEHRAN, Iran

UNAITWA Mlima Pickaxe. Unapatikana Kusini mwa Iran katika Jimbo la Isfahan, umbali wa maili 1.24 kutoka kilipo kinu cha nyuklia cha Natanz. Ulinzi ni wa hali ya juu, huku ujenzi wa barabara ya kuingia na kutoka katika Mlima huo ukifanyika mara kwa mara tangu mwaka 2020.

Kasi ya uwekezaji mkubwa katika eneo la Mlima huo imeongezeka mara dufu tangu mlipuko kuharibu iliyokuwa karakana ya nyuklia mjini Natanz. Karakana hiyo ililipuka Julai, 2020, ambapo mamlaka za Iran zilidai kulikuwapo na ‘mchezo mchafu’ katika tukio hilo.

Sasa, kinachoendelea katika Mlima Pickaxe kinaitia shaka Marekani, ikiamini kuwa Iran imeugeuza kuwa chimbo jipya na kubwa zaidi la utengenezaji wa silaha za nyuklia.

Moja ya Taasisi za masuala ya usalama mjini Washington iliwahi kueleza kuwa ndani ya Mlima huo kuna kinu cha nyuklia kinachopatikana umbali wa futi 330 kwenda chini.

Kwa mujibu wa Taasisi hiyo, katika mazingira hayo, ni ngumu kinu cha aina hiyo kufikiwa na shambulizi la anga. Hivi karibuni, Rais Donald Trump alikaririwa akisema vikosi vya jeshi la Marekani vitatekeleza mashambulizi katika Mlima huo.

“Tutalishambulia eneo hilo hivi punde. Hakuna wanachoweza kufanya kutuzuia,” alisema Rais Trump katika hotuba aliyoitoa akiwa Ikulu.

Kwa upande wake, Iran imemjibu ikisema nayo haitokaa kimya, na badala yake italipiza kisasi endapo Marekani itajaribu kutekeleza azima yao hiyo.

Hata hivyo, mamlaka za Iran hazijawahi kwa namna yoyote ile kueleza chochote juu ya kinachoendelea katika Mlima huo wa Pickaxe.

Lakini, Taifa hilo la Kiarabu halijaruhusu wapelelezi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomi (IAEA) kuingia na kupata taarifa za kinachofanyika.

Kwamba licha ya kuwapo kwa picha za setilaiti, si Marekani wala IAEA yenye ushahidi wa moja kwa moja juu ya kazi zinazofanyika katika Mlima huo.

Kukosekana kwa ushahidi na hatua ya Iran kuzuia wapepelezi kunaongeza utata na kuufanya Mlima Pickaxe kutupiwa jicho la karibu na jumuhiya za kimataifa.

Related articles

Recent articles