Na mwandishi wetu, Gazetini
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya, Mhashamu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki (AMECEA).
Uchaguzi huo umefanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA, uliowakutanisha Maaskofu kutoka nchi wanachama kujadili masuala mbalimbali yanayohusu kichungaji, uinjilishaji na maendeleo ya Kanisa Katoliki katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kuchaguliwa kwa Askofu Mkuu Nyaisonga kunatajwa kuwa hatua muhimu kwa Kanisa Katoliki Tanzania, kwani kunaonesha imani kubwa ambayo Maaskofu wa AMECEA wameweka katika uwezo wake wa uongozi. Akiwa Rais wa Shirikisho hilo, atakuwa na jukumu la kuratibu shughuli za AMECEA, kuimarisha ushirikiano kati ya Mabaraza ya Maaskofu wa nchi wanachama, kuendeleza utume wa Kanisa na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii na Kanisa katika ukanda huo.
AMECEA ni Shirikisho linalounganisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati, likiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa kichungaji, uinjilishaji, maendeleo ya kijamii na mshikamano wa Kanisa katika eneo hilo.
Waamini na viongozi mbalimbali wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania na nje ya nchi wameendelea kumpongeza Askofu Mkuu Nyaisonga kwa kuchaguliwa kwake, wakieleza matumaini yao kuwa uongozi wake utachangia kuimarisha utume wa Kanisa na kukuza mshikamano miongoni mwa Mabaraza ya Maaskofu wa AMECEA.
Kuchaguliwa kwake ni heshima kwa Kanisa Katoliki Tanzania na fursa ya kuendelea kutoa mchango katika uongozi wa Kanisa katika ngazi ya kikanda.


