23.1 C
New York

Tanzania yaidhinisha ombi la Sh trilioni 1.5 kupambana na UKIMWI…

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KAMATI ya Kitaifa ya Kuratibu na Kusimamia Fedha za Mfuko wa Dunia nchini Tanzania (TNCM) imeidhinisha rasmi ombi la Tanzania la ufadhili wa Mzunguko wa Nane wa Mfuko wa Dunia (Global Fund Grant Cycle 8 – GC8) lenye thamani ya dola za Marekani milioni 538.6 (takribani Sh trilioni 1.5), kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua Kikuu (TB) na Malaria pamoja na kuimarisha mifumo ya afya nchini.

Fedha hizo zinatarajiwa kutumika katika kipindi cha Januari 2027 hadi Desemba 2029, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Tanzania kuimarisha kinga, matibabu na huduma za afya kwa wananchi.

Uamuzi huo umefikiwa katika kikao maalumu cha TNCM kilichofanyika jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dk. Jim Yonazi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Dk. Yonazi alisema maandalizi ya ombi hilo yalianza Machi 13, 2026 na yalihusisha zaidi ya miezi minne ya mashauriano ya kitaifa, upangaji wa vipaumbele, mapitio ya kitaalamu na uhakiki wa nyaraka kabla ya kuidhinishwa.

Amesema mchakato huo ulihusisha ushiriki wa zaidi ya wadau 270 kutoka serikalini, mashirika ya maendeleo, taasisi za Umoja wa Mataifa, asasi za kiraia, sekta binafsi, taasisi za dini, watu wanaoishi na VVU pamoja na wataalamu wa afya.

“Kuidhinishwa kwa ombi hili ni matokeo ya ushirikiano mkubwa wa wadau waliowekeza muda, utaalamu na rasilimali kuhakikisha vipaumbele vya taifa vinazingatia mahitaji halisi ya wananchi na makundi yaliyoathirika zaidi,” amesema Dk. Yonazi.

Amesema uwekezaji wa Mfuko wa Dunia utawezesha Tanzania kuendelea kuzuia maambukizi mapya ya VVU, kuongeza upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV), kuimarisha kinga, uchunguzi na matibabu ya malaria, pamoja na kuboresha ugunduzi wa mapema na matibabu ya kifua kikuu.

Aidha, amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha mfumo wa afya ulio jumuishi, imara na endelevu, huku akiishukuru Sekretarieti ya Mfuko wa Dunia, wajumbe wa TNCM na wadau wote walioshiriki kufanikisha maandalizi ya ombi hilo.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TNCM, Kent Pius, amesema kamati hiyo itaendelea kuratibu ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha fedha za Mfuko wa Dunia zinatumika kwa ufanisi katika kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya kutokomeza UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria kama vitisho vya afya ya umma.

Related articles

Recent articles