20.5 C
New York

Serikali yatoa masharti ya kurejea kwa mikutano ya hadhara

Published:

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

SERIKALI imesema uamuzi wa kusitisha kwa muda mikutano ya hadhara umetokana na sababu za kiusalama baada ya vyombo vya ulinzi na usalama kubaini kuwepo kwa mipango ya watu wenye nia ovu ya kuvuruga amani na usalama wa nchi.

Akizungumza Julai 22, 2026, wakati wa ziara yake katika Soko la Machinga na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema jukumu la msingi la Serikali ni kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unalindwa wakati wote.

Amesema Tanzania ina vyombo imara vya ulinzi na usalama vinavyofanya kazi ya kubaini na kudhibiti vihatarishi kabla havijasababisha madhara kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Polisi walibaini kuwepo kwa mipango ya watu wenye nia ovu. Serikali ina wajibu wa kulinda raia na mali zao. Hii ni nchi yenye misingi ya kikatiba, lakini tunapolinda usalama wa wananchi hakuna mzaha. Ikikatazwa, imekatazwa,” amesema Msigwa.

Ameongeza kuwa mikutano ya hadhara itaruhusiwa mara baada ya vyombo vya ulinzi na usalama kujiridhisha kuwa mazingira ya usalama yamerudi kuwa tulivu na hakuna tena vihatarishi vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi.

Msigwa alikumbusha kuwa matukio ya kiusalama yaliyotokea Oktoba 29 mwaka jana yalisababisha kupotea kwa maisha ya baadhi ya wananchi na hasara ya mali, hivyo Serikali haitaruhusu hali kama hiyo kujirudia.

“Hatutaruhusu yaliyotokea mwaka jana yajirudie tena. Watu walipoteza maisha na Watanzania walipata hasara. Never and never again,” amesema.

Akizungumzia sekta ya afya, Msigwa amesema Serikali inaendelea kutekeleza mfumo wa Huduma za Afya kwa Wote, ambao utasaidia kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya.

Kuhusu suala la Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, amesema Serikali inaendelea kutafakari namna ya kutekeleza hoja na mapendekezo yaliyotolewa na Jumuiya ya Madola kuhusu suala hilo.

Aidha, amewataka vijana kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizowekwa na Serikali, ikiwemo mikopo, ruzuku, kilimo, ufugaji na biashara, badala ya kushiriki vitendo vya vurugu.

Amesisitiza kuwa Serikali imeendelea kujenga masoko na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na biashara ili kuwawezesha vijana kujiajiri na kuongeza kipato.

“Kijana huna sababu ya kulalamika. Fanya biashara, lima au fuga. Acheni kupoteza muda kuhamasishana kufanya vurugu. Hakuna nchi yoyote iliyoendelea kwa watu kukaa bila kufanya kazi. Nimetoka Ufaransa, watu wanafanya kazi kwa bidii,” amesema Msigwa.

Related articles

Recent articles