Na mwandishi wetu, Gazetini
HATIMAYE mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-26, Yanga, wamempa kazi raia huyo wa Afrika Kusini kuwa kocha wao mpya.
Taarifa za Manqoba Mngqithi kutua Yanga zinakuja saa chache tu baada ya kocha wa zamani wa timu hiyo kujiunga na AS FAR Rabat ya Morocco.
Mngqithi mwenye umri wa miaka 55, si jina geni katika soka la Afrika Kusini kwani ametoka kufanya kazi na Golden Arrows ya Ligi Kuu nchini humo.
Aliondoka Arrows baada ya timu hiyo kumaliza msimu ikiwa nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi.
Akiwa na Mamelodi Sundown, Amazulu, Chippa United na Arrows kwa nyakati tofauti, Mngqithi alibeba vikombe 10, likiwamo la Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Alipoajiriwa na Mamelodi kama kocha msaidizi mwaka 2013, aliambatana na Rhulani Mokwena kwenye majukumu hayo klabuni hapo.
Mwaka 2020, wote walipandishwa ngazi kushika nafasi ya kocha mkuu, ambapo waliweza kuipa Mamelodi mataji mawili ya Ligi Kuu.
Baadaye, Mokwena alikabidhiwa benchi kama kocha mkuu, kisha Mngqithi akawa msaidizi wake.
Mamelodi walipomfukuza Mokwena mwaka 2024, mabosi wa klabu hiyo walimpa kibarua Mngqithi.
Hata hivyo, alidumu kwenye benchi kwa miezi kadhaa tu, kabla ya kufungashiwa virago Desemba, 2024, baada ya mfululizo wa matokeo mabaya.
Akiwa na leseni ya Diploma ‘A’ ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), ni kocha anayeamini zaidi katika mfumo wa 4-3-3.
Baadhi ya makocha wakubwa duniani wanaotegemea mfumo huo wa 4-3-3 ni Pep Guardiola, Jurgen Klopp, Mikel Arteta, na Zinedine Zidane.
Muundo wa mfumo huo ni mabeki wanne – wawili wa kati kulinda boksi na wawili wa pembeni wanaozuia na kuisadia timu kupandisha mashambulizi.
Kwa viungo watatu, mmoja anakuwa mlinzi (namba 6), kisha wawili wanasimama juu yake ili kutawala eneo la katikati ya uwanja.
Eneo la mwisho linakuwa na washambuliaji watatu, mmoja akisimama (straika) na wawili wakifanya majukumu ya kuisumbua safu ya ulinzi ili kutengeneza nafasi za kufunga.


