28.9 C
New York

Mastaa wa soka na ‘ulevi’ wa mbio za magari

Published:

LONDON, Uingereza

KWA miaka mingi, wachezaji wa kandanda wamekuwa na ukaribu mkubwa na mchezo wa mashindano ya mbio za magari.

Mbali na mambo mengine, mara kadhaa nyota hao wamekuwa wakitumia mapumziko yao kuhudhuria michuano ya mbio za magari.

Kupata picha halisi, ni kama ilivyo kwa wanamuziki wa Marekani, ambao wengi wao ni ‘walevi’ wa Ligi Kuu ya Kikapu nchini humo (NBA).

LIONEL MESSI

Kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu (2026), supastaa huyo wa timu ya soka ya Taifa ya Argentina alionekana kwenye mashindano ya mbio za magari ya Miami Grand Prix.

Aliweza pia kuitembelea timu ya Mercedes na kupiga stori na madereva wake, wakiwamo mastaa Kimi Antonelli na George Russell.

PELE

Ndiye mwanasoka pekee kuwahi kutwaa Kombe la Dunia mara tatu (1958, 1962 na 1970). Taji la kwanza alibeba akiwa na umri wa miaka 17.

Pele (sasa marehemu), alikuwa shabiki mkubwa wa mbio za magari. Alihudhuria michuano ya Grand Prix ya Brazil mwaka 2002, ambapo dereva raia wa Ujerumani, Michael Schumacher, alitwaa ubingwa.

Mwaka 2006, ndiye aliyekabidhi tuzo baada ya waandaaji wa Formula One kumtambua Schumacher kwa mchango wake kwenye mashindano hayo ya mbio za magari.

KYLIAN MBAPPE

Mshambuliaji huyo aliibeba mabegani Ufaransa ilipotwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2018. Alifunga mabao manne, likiwamo moja la fainali na kuwa Kinda Bora wa michuano.

Mbappe humwambii kitu kwenye mbio za magari. Amekuwa akihudhuria wikiendi nyingi za michuano ya Grand Prix, ikiwamo inayofanyika Monaco, Ufaransa.

Mwaka 2024, alihudhuria mashindano yaliyomalizika kwa Charles Leclerc kunyakua ubingwa.

RONALDO DE LIMA

Mkongwe wa soka la Brazil, ambaye alitwaa Kombe la Dunia mara mbili (1994 na 2002). Nje ya soka, ni mpenzi mkubwa wa mbio za magari.

Tangu mwaka 1999, Ronaldo amekuwa mfuatiliaji mzuri wa michuano ya Grand Prix. Amekuwa akialikwa na klabu za Ferrari na Red Bull katika michuano inayofanyika Abu Dhabi.

DIEGO MARADONA

Alikuwa wa moto katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1986, akifunga mabao matano, asisti nne na kuiwezesha Argentina kutwaa ubingwa.

Maradona (sasa marehemu), alikuwa kindakindaki wa mbio za magari, ikiwamo kuhudhuria mashindano ya Monaco Grand Prix mwaka 1995.

ZINEDINE ZIDANE

Dereva maarufu wa mchezo wa mbio za magari, Pierre Gasly, aliwahi kusema huwa anatumia namba 10 kutokana na mapenzi yake kwa Zidane.

Zidane aliyetwaa Kombe la Dunia mwaka 1998, akifunga mara mbili katika mechi ya fainali (dhidi ya Brazil), ni shabiki wa timu ya mbio za magari ya Alpine na alihudhuria sherehe ya utambulisho wa magari yao mapya mwaka 2023.

MARIO GOTZE

Wakati Ujerumani inatwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2014, Gotze ndiye aliyefunga bao la ushindi katika fainali yao dhidi ya Argentina.

Nje ya soka, Gotze ni shabiki wa mbio za magari na mwaka huu (2026) alihudhuria mashindano ya Monaco Grand Prix akiwa na wakongwe wenzake, Lukas Podolski na Mats Hummels.

ALESSANDRO DEL PIERO

Alifunga bao lililoipeleka timu ya Taifa ya Italia hatua ya fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2006, kisha akafunga penalti katika mchezo wa fainali (dhidi ya Ufaransa) na kutwaa ubingwa.

Del Piero, nyota wa zamani wa Juventus, ameonekana mara kadhaa kwenye mashindano ya Grands Prix, hasa Yale yanayofanyika Monza, Italia.

ROBERTO CARLOS

Beki wa kushoto wa zamani wa timu ya soka ya Taifa ya Brazil ‘Selecao’. Alistaafu akiwa ametwaa mara mbili ubingwa wa Kombe la Dunia (1998 na 2002).

Tangu alipotundika daluga, amekuwa hakosekani katika mashindano ya mbio za magari, yakiwamo ya Grand Prix yanayofanyika Brazil, Hispania, Italia na Marekani.

Related articles

Recent articles