Na Ramadhan Hassan, Dodoma
HOSPITALI ya Benjamin Mkapa (BMH), kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), imeandika historia kwa kufanikisha kwa mara ya kwanza kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Burundi, hatua inayoimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkurugenzi wa BMH, Prof. Abel Makubi, alisema mafanikio hayo yanaashiria hatua mpya katika utoaji wa huduma za afya za kibingwa na utekelezaji wa mkakati wa kukuza tiba utalii nchini.
“Ni hatua ya kihistoria. Hii ni mara ya kwanza BMH kwa kushirikiana na JKCI kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka nje ya Tanzania. Mafanikio haya yanaonyesha uwezo wa wataalamu wetu na yanaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa kutoka ndani na nje ya nchi,” amesema Prof. Makubi.
Alisema ushirikiano kati ya BMH na JKCI utaendelea kuimarishwa ili kupanua huduma za kibingwa, kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi na kuvutia wagonjwa kutoka mataifa jirani kupata matibabu nchini kwa gharama nafuu.
“Kipaumbele chetu ni kuona Tanzania inakuwa kituo cha huduma za moyo katika ukanda huu. Badala ya wananchi wetu na wa nchi jirani kusafiri kwenda mataifa ya mbali kutafuta matibabu, wanapaswa kupata huduma hizo hapa nchini kwa ubora unaokidhi viwango vya kimataifa,” amesema.
Bingwa wa Upasuaji wa Moyo na Kifua, Dk. Ahmed Toure, alisema watoto waliopatiwa matibabu walikuwa na matatizo ya kuzaliwa ya muundo wa moyo (congenital heart defects), yaliyokuwa yakisababisha moyo kushindwa kusukuma damu kwa ufanisi au damu kutofika kwenye mapafu kwa kiwango kinachohitajika.
Alifafanua kuwa iwapo watoto wenye matatizo hayo hawatapatiwa matibabu mapema, wanaweza kupata madhara makubwa ya mapafu na moyo, hali inayoweza kupunguza uwezekano wa mafanikio ya matibabu baadaye.
“Watoto wengi wanapaswa kufanyiwa upasuaji ndani ya miezi sita hadi mwaka mmoja wa maisha. Wakipata matibabu kwa wakati, wana nafasi kubwa ya kuishi maisha marefu na yenye ubora,” amesema.
Mratibu wa Tiba Utalii Tanzania, Dk. Asha Mahita, alisema mafanikio hayo yanaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za tiba utalii barani Afrika.
Alisema kuwahudumia watoto kutoka Burundi ni uthibitisho wa kuongezeka kwa uwezo wa nchi kutoa huduma za kibingwa zinazovutia wagonjwa kutoka mataifa mengine.
Kwa upande wake, Bingwa Mbobezi wa Upasuaji wa Moyo kwa Watoto kutoka JKCI, Dk. Godwin Godfrey, alisema ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili unachangia kuongeza ujuzi wa wataalamu, kuboresha ubora wa huduma na kupanua fursa za matibabu kwa wagonjwa wengi zaidi.
Naye daktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Gitega nchini Burundi, Dk. Nzitunga Aimee Jean Carmen Octavie, aliishukuru Tanzania kwa kuwapatia watoto hao huduma salama na za kiwango cha juu, akisema hatua hiyo imeimarisha ushirikiano wa sekta ya afya kati ya nchi hizo mbili.
Mzazi wa mmoja wa watoto waliopatiwa matibabu, Shedrack Nzigiyimana, alisema afya ya mtoto wake imeimarika baada ya upasuaji na kuishukuru Serikali ya Tanzania pamoja na timu ya madaktari wa BMH na JKCI kwa huduma waliyoipata.


