MEXICO CITY, Mexico
FAINALI za Kombe la Dunia za mwaka huu (2026) zinaendelea kuchanja mbuga, huku baadhi ya timu zikiwa zimeshatinga hatua ya 16 Bora.
Baadhi ya mechi kali za hatua hiyo ni ile itakayozikutanisha England ‘Three Lions’ na Mexico ‘El Tri’, ambao ni wenyeji wa michuano kwa kushirikiana na Marekani na Canada.
Mchezo huo wa kusaka tiketi ya kwenda robo fainali utachezwa Jumapili ya wiki hii (Julai 5, 2026) katika Uwanja wa Mexico City.
Mexico wamefika hapa baada ya ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya Ecuador katika mchezo wa hatua iliyopita ya 32 Bora.
Kwa upande wake, England ilitinga 16 Bora baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DCR).
Kwa mujibu wa rekodi, England na Mexico zinakutana kwa mara 10 katika historia ya mchezo wa soka.
Katika mechi tisa zilizopita, England wameongoza kwa ushindi mara sita, wakifungwa mbili, na sare moja.
England imefunga jumla ya mabao 23 katika mechi zote ilizowahi kukutana na Mexico, huku ikiruhusu mara nne pekee nyavu zake kutikiswa.


