WASHINGTON DC, Marekani
JULAI 4, 2026, Marekani itasherehekea miaka 250 tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1776 kutoka kwa Uingereza.
Hata hivyo, ‘birthday’ inakuja wakati Taifa hilo likiwa limegawanyika kutokana na sera za Rais aliyeko madarakani, Donald Trump. Wapo wanaomuunga mkono na wengine kumpinga.
Betsy Halsey (63), ni mwalimu mstaafu. Kwa upande wake, hakubaliani na utawala wa Rais Trump, hivyo haoni sababu ya kuungana na Wamarekani wengine kusherehekea Siku ya Uhuru.
“Sitaki kuungana na watu ambao hawajali kuhusu hatima ya nchi yetu,” amesema Halsey, ambaye ni mkazi wa Doylestown, Pennsylvania.
Pennsylvania ni moja ya maeneo ambayo Rais Trump hana ushawishi mkubwa, ikikumbukwa kuwa alipata kura zisizozidi 300 katika Uchaguzi uliomrejesha madarakani mwaka 2024.
Hata hivyo, mtazamo wa Halsey unatofautiana na alionao mkazi mwenzake wa Pennsylvania, Langhorne Manor.
Manor (70), anaamini Marekani imepiga hatua kubwa na inang’ara zaidi chini ya uongozi wa Rais Trump.
Kwa upande wake, amesema ataiadhimisha Siku ya Uhuru (Julai 4) kwa kufanya sherehe ya kula na kunywa na ndugu, jamaa na marafiki.
“Mtu masikini zaidi hapa Marekani ana maisha mazuri kuliko matajiri wa baadhi ya nchi,” amesema Manor.
Hata hivyo, utafiri wa Gazeti la Reuters umebaini kuwa kati ya watu watano nchini Marekani, mmoja haoni sababu ya kufurahia Siku ya Uhuru chini ya Rais Trump.
Aidha, wawili kati ya watano wanaonesha wasiwasi wa Marekani kupoteza nguvu yake kiuchumi na kisiasa baada ya miaka 250 ijayo.
Licha ya kuwapo kwa hisia tofauti, Rais Trump ameipa uzito mkubwa Siku ya Uhuru, ambapo mwaka jana (2025) aliunda ‘Freedom 250’, ushirikiano wa Serikali na taasisi binafsi kwa ajili ya maandalizi ya Siku ya Uhuru.
Rais Trump alikuja na Kamati hiyo, licha ya kuwapo kwa ‘America250’, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikiandaa sherehe za Siku ya Uhuru.
Baada ya Rais Trump kuizindua Kamati yake kwa sherehe iliyoambana na mkutano, kana kwamba ni kampeni, wakosoaji wake wamesema Rais Trump amejimilikisha na kuingiza siasa katika tukio nyeti la Siku ya Uhuru.
Profesa Tabitha Dell’Angelo ni miongoni mwa walioweka wazi, kwamba hatosherehekea Siku ya Uhuru, akisema
“Naipenda nchi yangu na najivunia kuwa Mmarekani. Lakini aina ya sherehe haionekani ni za Marekani, bali za Trump.”
Mwanaharakati na mwandishi wa vitabu, Doreen Stratton, anasema babu yake alikuwa mmoja ya watu weusi waliokuwa wakiishi Pennsylvania wakati Marekani inapata uhuru mwaka 1776.
Kwa mtazamo wake, haoni cha kufurahia Julai 4 kwa kuwa watu weusi nchini Marekani bado wanapitia changamoto za ubaguzi wa rangi chini ya utawala wa Rais Trump.


