Na Hassan Mwasha, Gazetini
SIMBA ikiwa nyumbani katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamhuyo, imeondoka na pointi zote tatu baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida Black Stars.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-26 umechezwa leo Juni 27, 2026, huku Simba ikipata bao lake la kwanza dakika ya 31, mfungaji akiwa ni Elie Mpanzu.
Wekundu wa Msimbazi walirudi katika nyavu za Singida katika dakika ya 60, safari hii Mpanzu raia wa DRC akitoa asisti kwa Anicet Oura kutoka Ivory Coast.

Kwa maana hiyo, Mpanzu amefikisha pasi 10 za mabao (asisti) tangu msimu huu wa Ligi Kuu Bara ulipoanza.
Katika hatua nyingine, ushindi wa leo umeifanya Simba kubaki nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kufikisha pointi 70, ikiendelea kudaiwa mbili na Yanga iliyoko kileleni.


