DRC, Congo
JAMHURI ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imefungua kesi dhidi ya Rwanda katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) iliyoko The Hague, Uholanzi, ikiitaka mahakama hiyo kuiwajibisha Rwanda kwa madai ya ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Hatua hiyo imethibitishwa jana Ijumaa na Waziri wa Sheria wa DRC, Guillaume Ngefa Atondoko Andali, aliyesema serikali ya Kinshasa imeamua kutumia njia za kisheria kama sehemu ya dhamira yake ya kutatua migogoro kwa amani, kwa kuzingatia misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa waziri huyo, hatua ya kuwasilisha shauri hilo inalenga kuhakikisha haki inatendeka kwa waathirika wa madai hayo, huku serikali ya DRC ikiendelea kuheshimu taratibu na mchakato wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki.
“Hii ni sehemu ya dhamira yetu ya kutafuta suluhisho la migogoro kwa njia za amani na kwa kuzingatia sheria za kimataifa,” amesema Andali. Hadi kufikia sasa, serikali ya Rwanda haijatoa tamko rasmi kuhusu kesi hiyo.
Hata hivyo, wachambuzi wa sheria za kimataifa wameeleza kuwa shauri hilo linaweza kukumbana na changamoto za kisheria, hususan kuhusu iwapo Mahakama ya Kimataifa ya Haki ina mamlaka ya kulisikiliza bila Rwanda kutoa ridhaa yake au kuwepo kwa msingi wa kisheria unaoipa mahakama mamlaka ya kushughulikia mgogoro huo.
Kesi hiyo inakuja wakati uhusiano kati ya DRC na Rwanda ukiendelea kuwa wa mvutano, huku Kinshasa ikiendelea kuituhumu Kigali kwa kuhusika na machafuko yanayoendelea mashariki mwa Congo, madai ambayo Rwanda imekuwa ikiyakanusha.


