20.7 C
New York

Yanga, Azam zaacha historia ya ‘vichwa’ CCM Kirumba

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

INAWEZA kuumiza kichwa kukumbuka mechi ya aina hii; Yanga dhidi ya Azam, ambayo ilimalizika kwa jumla ya mabao matano na yote yakifungwa kwa kichwa.

Ndicho kilichotokea katika nusu fainali ya Kombe la FA iliyochezwa Juni 21, 2026, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Dakika 120 za mtanange huo wa pili, baada ya nusu fainali ya kwanza kati ya Simba na Coastal, zilimalizika kwa Yanga kutandikwa mabao 3-2 na matajiri hao wa Chamazi, Azam.

Mabao yote yalifungwa kwa staili moja, mipira ya vichwa, ambapo ya Azam ilitangulia kupitia kwa Himid Mao (Dk. 27), kisha Prince Dube akaisawazishia Yanga kwa staili hiyo hiyo (Dk. 66) kupitia krosi ya Allan Okello.

Lameck Lawi aliyetokea benchi, naye alifunga kwa kichwa (Dk. 84), akiunganisha mpira wa kona wa Feisal Salum, kama ambavyo Bakari Nondo naye alijibu kwa staili hiyo (Dk. 87) akitumia asisti ya Okello.

Katika dakika ya 112, Azam walirudi kwenye nyavu za Yanga, safari hii straika raia wa DRC, Bola Kitambala, akifunga pia kwa kichwa.

Matajiri wa Chamazi, Azam, sasa wanajiandaa kuikabili Simba katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo ambayo msimu huu inadhaminiwa na Benki ya CRDB.

Simba, kwa upande wao, walitinga kibabe hatua ya hiyo baada ya ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Related articles

Recent articles