Na mwandishi wetu, Gazetini
BAADA ya kuitazama Azam ikiifunga Yanga na kutinga fainali ya Kombe la FA, mashabiki wa Simba wameonesha kutoridhishwa na matokeo hayo.
Yanga imepoteza mbele ya Azam kwa kichapo cha mabao 3-2, mchezo uliochezwa leo Juni 21, 2026, katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
“Sisi tulimtaka ‘my’ wetu. Ila hata hao Azam siyo mbaya. Tunawapiga na kurejesha heshima Msimbazi.
“Hata kwenye Ligi, wakae kwa kutulia. Wakijichanganya tu, tunapita nao,” anasema Ally Mtumwa, mmoja ya mashabiki wa Simba, mkazi wa Tandale kwa Mtogole jijini Dar es Salaam.
Azam ilikuwa ya kwanza kutangulia kwa bao la kichwa la Himid Mao, kabla ya Prince Dube kuisawazishia Yanga.
Beki wa kati wa Yanga, Bakari Nondo, aliifunga bao dakika za mwisho, akijibu bao la Lameck Lawi wa Azam, hivyo dakika 90 kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Matokeo hayo yalilazimisha kuongezwa dakika 30 za kucheza, na ndipo straika raia wa DRC, Kitambala, alipofunga ukingoni mwa mchezo huo.
Simba walishatangulia mapema hatua ya fainali baada ya ushindi wao wa mabao 4-0 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa jana Juni 20, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abedi jijini Arusha.


