WASHINGTON DC, Marekani
IDADI ya vifo vya wahamiaji wanaoshikiliwa katika magereza nchini Marekani imeongezeka mara dufu tangu Rais Donald Trump aliporejea madarakani.
Kwa mujibu wa Gazeti la Reuters, idadi ya sasa ni mara mbili zaidi ya ilivyokuwa kabla ya Rais huyo kushinda Uchaguzi wa mwaka 2024.
Takwimu za jumla zinaonesha kuwa wahamiaji 50 wameshapoteza maisha tangu Rais Trump alipoanzisha kampeni ya ‘kamatakamata’ Januari, 2025.
Kati ya mwaka 2000 hadi 2024, magereza ya Marekani yalikuwa na wastani wa kifo kimoja kwa siku kati ya wahamiaji 3,848.
Kwa sasa, tangu Rais Trump arejee Ikuku, ni kifo kimoja kwa siku kati ya wahamiaji 1,630 wanaoshikiliwa.
Gereza la Indiana, ambalo linasifika kwa kiwango kikubwa cha ulinzi, limetajwa kuongoza kwa vifo vingi vya wahamiaji chini ya utawala wa Rais Trump.
Katika Gereza la Pennsylvania, mwanaume raia wa China, ambaye aliwahi kujaribu kujiua, alikutwa hivi karibuni akiwa amejinyonga.
Gereza jingine la New York lilishuhudia mwanaume raia wa Honduras alikutwa amefariki, chanzo kikiwa ni kukosa matibabu ya dharura katika tatizo lake la ugonjwa wa moyo.
Magonjwa ya moyo yameripotiwa kuongoza kwa idadi ya vifo, huku mamlaka zikishutumiwa kwa kutokuwapa huduma bora za afya wahamiaji wanaoshikiliwa magerezani.


