NEW YORK, Marekani
NI kwa mujibu wa Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa (UN), kwamba takribani visa 10,000 vya unyanyasaji wa kingono viliripotiwa katika maeneo mbalimbali duniani mwaka 2025.
UN imeeleza kuwa idadi hiyo ni mara mbili ya ile ya mwaka 2024, huku matukio yakihusisha wanawake kubakwa, kutekwa na kufanywa watumwa wa kingono.
Katika ripoti hiyo, UN imeyataja maeneo yanayokabiliwa na migogoro ya kisasa, ikiwamo Afrika, Mashariki ya Kati na Ulaya, kuwa ndiyo yenye matukio mengi.
Hata hivyo, Mjumbe Maalumu wa UN, Pramila Patten, amesema: “Idadi (ya matukio) iliyoko kwenye ripoti hii haitoi picha kamili, bado kuna mengi yasiyoonekana na yasiyoripotiwa.”
Ripoti hiyo imetaja maeneo 21 yenye hali mbaya ya usalama duniani, ikieleza kuwa yamekuwa kichaka cha ukatili wa kijinsia dhidi ya wasichana na wanawake wenye umri kati ya mwaka mmoja hadi miaka 70.


