21.2 C
New York

Usiyoyajua kuhusu matumizi ya mirungi

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MATUMIZI ya mirungi yana historia ndefu barani Afrika, yakitajwa kuanza miaka mingi iliyopita katika nchi za Ethiopia, Eritrea, Kenya na Somalia.

Mirungi ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa ‘Catha edulis’, ambao una kemikali za ‘cathinone’ na ‘cathine’.

Kutoka eneo moja na jingine, mirungi imekuwa ikipewa majina tofauti, yakiwamo ‘gomba’, ‘veve’, ‘miraa’, ‘kangeta’, ‘mkokaa’, ‘colombo’, ‘asili’, ‘mbaga’ na ‘alenle’.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya hapa nchini (DCEA) inaeleza kuwa wanaume walikuwa wakitumiaji wakubwa lakini wanawake wameingia kwa wingi katika miaka ya hivi karibuni.

KILIMO CHA MIRUNGI

Kupitia tovuti yake, DCEA inaeleza kuwa kwa Tanzania, mirungi hustawi na hupatikana kwa wingi katika mikoa ya Kilimanjaro- Same, Tanga- Lushoto na Arusha- Mlima Meru.

Pia, kiasi kikubwa cha mirungi huingizwa nchini kwa ‘njia za panya’ ikitokea nchi jirani ya Kenya, ambako sheria hazibani kwa kuwa ni zao halali la biashara.

MADHARA KWA WATUMIAJI

DCEA inaeleza kuwa matumizi ya mirungi huongeza kasi ya mapigo ya moyo, hivyo husababisha shinikizo la damu, kiharusi na hata kifo.

Pia, ni chanzo cha vidonda vya utumbo mdogo, saratani ya mdomo, koo na tumbo, upungufu wa hamu au kushindwa kudumu kwenye tendo la ndoa kwa muda mrefu, na kupunguza ubora wa mbegu za kiume kunakoweza kusababisha ugumba.

Mtumiaji hukosa usingizi, hamu ya kula, kupungua uzito, upungufu wa maji mwilini, kukosa choo, ugonjwa wa bawasiri, sonona, kuozesha meno, kuharibu ufanisi wa ini.

Kwa wanawake wajawazito, hatari iliyopo ni kuzaliwa kwa watoto wenye uzito mdogo ambao huweza kukataa kunyonya kutokana na ladha ya maziwa kubadilishwa na viuatilifu vinavyotumika kwenye kilimo cha mirungi.

SHERIA ZINASEMAJE?

DCEA inaweka wazi kuwa mirungi ni haramu kwa sheria za hapa nchini. Kujihusisha kwa namna yoyote na mirungi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, n.k.) ni kosa la jinai na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha.

Baadhi ya nchi za Ulaya ambazo awali ziliruhusu matumizi ya mirungi zimeanza kuiharamisha baada ya kujiridhisha juu ya madhara yake.

Related articles

Recent articles