19.8 C
New York

Sheria ya malezi ya watoto inayotesa ‘ma-ex’ Japan

Published:

TOKYO, Japan

KABLA ya kufanyiwa marekebisho Aprili Mosi, 2026, Sheria ya Malezi nchini Japan ilimtaka mzazi mmoja pekee kumiliki mtoto/watoto pale ilipotokea ndoa au mahusiano kuvunjika.

Kwamba mzazi atakayewahi kumchukua mtoto wakati wa kuachana ndiye atakayekuwa na mamlaka yote, ikiwamo kumzuia kabisa ‘ex’ wake kujishugulisha na malezi.

Ni katika mazingira hayo, wanaume, kama ilivyo kwa wanawake wengi nchini Japan, walilazimika kuanza upya kutafuta watoto baada ya kupoteza haki ya kumiliki wale waliowapata katika mahusiano yaliyovunjika.

John Deng anayetokea Hong Kong, ambaye amekuwa Japan kwa miaka 22, alipoteza ukaribu na watoto wake wawili – binti mwenye umri wa miaka 10 na wa kiume wa miaka 8 – tangu alipovunja ndoa yake ya awali.

Deng anasema mke wake aliondoka na watoto hao na tangu hapo hakuweza kuwaona wala kuwasiliana nao kwa kuwa Sheria ya malezi ya Japan ilimtambua mzazi mmoja tu baada ya ndoa/mahusiano kuvunjika

“Nilijiona ni mtu niliyekosa msaada. Nilihuzunika sana na kukerwa na uwepo wa sheria iliyoruhusu hali hii kutokea,” alisema Deng na kuongeza kuwa mke wake wa zamani alizuia hata mawasiliano ya simu kati yake na watoto.

Kwa sasa, mambo yamebadilika. Mabadiliko ya Sheria yameleta mazingira rafiki kwa wenza kushirikiana katika kulea watoto hata kama walishindwa kuendelea na mahusiano yao.

Deng, kwa upande wake, mabadiliko hayo yamemrejeshea si tu tabasamu, bali pia tumaini lililopotea kwenye uso wake kwa miaka mingi. “Kwa sasa, nina makazi mawili, moja hapa Tokyo na mengine ni umbali wa saa moja tu kufika wanapoishi watoto wangu,” amesema.

Hata hivyo, mabadiliko ya Sheria kuruhusu wenza wa zamani kushirikiana katika malezi ya watoto yamepokelewa kwa maoni tofauti, yakiwamo ya kukosoa hatua hiyo.

Mtazamo wa wakosoaji ni kwamba wapo wanaume au wanawake waliokimbia ndoa au mahusiano kutokana na vitendo vya unyanyasaji, hivyo kuwakutanisha tena na wenza wao kwa kigezo cha malezi ya watoto ni kutokuwatendea haki.

Related articles

Recent articles