ACCRA, Ghana
SERIKALI ya Ghana imepeleka ndege maalumu nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kuchukua raia wake 300 wakati huu wa machafuko yanayoendelea.
Baadhi ya wananchi wa Afrika Kusini wamekuwa wakifanya vurugu kwa kile wanachosema wageni wamechukua nafasi za ajira, pia wingi wao umeathiri ubora wa huduma za afya.
Katika matukio hayo ya vurugu, ambayo Serikali ya Afrika Kusini imeyalaani, wageni wamekuwa wakipigwa, kuporwa mali zao na hata kuuawa.
Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ghana, imeeleza kuwa ndege waliyotuma nchini Afrika Kusini imewarejesha raia 300 mjini Accra.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mamlaka za Afrika Kusini, ni 10 pekee kati ya hao 300 waliokuwa wakiishi nchini humo kwa kufuata taratibu za uhamiaji.
Aidha, Ubalozi wa Ghana nchini Afrika Kusini umeeleza kuwa bado kuna raia wake 800 wanapaswa kuondoshwa nchini humo, hivyo ndege nyingine itaanza safari mwishoni mwa wiki hii.