CATALUNYA, Hispania
HATIMAYE Arsenal imetinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ni baada ya ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Atletico Madrid, mchezo uliochezwa usiku wa jana Mei 5, 2026.
Ilikuwa ni nusu fainali ya pili ya michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) iliyochezwa Emirates baada ya ile ya kwanza iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 jijini Madrid.
Washika Bunduki hao wa Kaskazini mwa Jiji la London walipata ushindi huo kupitia bao la mshambuliaji wake raia wa England, Bukayo Saka.
Kwa ushindi huo, vijana hao wa kocha Mikel Arteta wameweka rekodi tatu, kama zilivyoainishwa na mtandao wa takwimu wa OptaJoe.
Mosi, hii inakuwa mara ya kwanza kwa Arsenal kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu ilipofika hatua hiyo mwaka 2006.
Pili, Arsenal ndiyo timu pekee ambayo haijafungwa msimu huu wa Ligi ya Mabingwa. Washika Bunduki hao wameshuka dimbani mara 14.
Tatu, kwa kuifunga Atletico, Arsenal wameifikia rekodi yao ya kushinda mechi nyingi (41) za mashindano mbalimbali ndani ya msimu mmoja.


