Na mwandishi wetu, Gazetini
DUNIA inaendelea kushuhudia mageuzi makubwa ya teknolojia yanayobadilisha namna shughuli mbalimbali zinavyotekelezwa kila siku, huku sehemu kubwa ya maendeleo hayo ikilenga kurahisisha kazi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikifanywa na binadamu.
Ingawa hapo awali maendeleo hayo yalipokelewa kwa matumaini makubwa kama hatua ya kurahisisha maisha na kuongeza ufanisi, sasa kwa baadhi ya watu yameanza kuonekana kama tishio kutokana na kuendelea kupunguza nafasi za ajira katika sekta mbalimbali.
Moja ya teknolojia zinazozua mjadala mkubwa ni akili mnemba (AI), ambayo imeanza kutumika kwa kiwango kikubwa kama mbadala wa nguvu kazi ya binadamu, hali inayochangia kampuni nyingi kupunguza wafanyakazi wake.
Kampuni ya Meta imetangaza kuwa itapunguza takribani asilimia 10 ya wafanyakazi wake, sawa na watu karibu 8,000, katika hatua mpya ya kupunguza ajira inayochochewa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji mkubwa kwenye teknolojia ya akili bandia (AI).
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo, pia nafasi za kazi zipatazo 6,000 ambazo zilikuwa wazi zitafutwa, huku mchakato wa kupunguza wafanyakazi ukitarajiwa kuanza rasmi Mei 20.
Ofisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Meta, Janelle Gale, amesema hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa kampuni na kusaidia kufidia gharama za uwekezaji mwingine unaoendelea kufanywa.
Meta imekuwa miongoni mwa kampuni zinazoongoza kwa matumizi makubwa katika AI, ikitumia dola bilioni 72.2 mwaka 2025 kwa miundombinu ya data na teknolojia ya AI, huku matumizi hayo yakitarajiwa kufikia angalau dola bilioni 115 mwaka 2026.
Mbali na uwekezaji huo, kampuni hiyo imeendelea kuajiri wataalamu wa AI na kununua kampuni changa za teknolojia ili kuimarisha ushindani wake dhidi ya kampuni kama OpenAI.

Mkurugenzi Mtendaji wa Meta, Mark Zuckerberg, amesema mwaka 2026 utakuwa kipindi ambacho AI itabadilisha kwa kiasi kikubwa namna watu wanavyofanya kazi, akibainisha kuwa miradi iliyokuwa ikihitaji timu kubwa sasa inaweza kufanywa na mtu mmoja mwenye ujuzi mkubwa.
Wafanyakazi wa Marekani watakaoathirika na mpango huo watapatiwa malipo ya wiki 16 ya mshahara pamoja na wiki mbili za ziada kwa kila mwaka waliotumikia. Hatua hiyo inakuja wakati kampuni nyingi za teknolojia duniani zikiendelea kupunguza wafanyakazi kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya AI katika shughuli za biashara.


