DAKAR, Senegal
RAIA wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, ametia saini kupitisha sheria mpya inayohukumu kifungo cha hadi miaka 10 gerezani kwa wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Sheria hiyo pia inapiga marufuku na kuwatia hatiani wale wote wanaotoa ufadhili wa fedha kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Kubainika kufadhili vitendo hivyo ni kosa linalogharimu kifungo cha miaka mitatu hadi saba gerezani, kwa mujibu wa sheria mpya hiyo.
Ikumbukwe, sheria hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Faye na Waziri Mkuu wake, Ousmane Sonko.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Kitengo cha Haki za Binadamu cha Umoja wa Mataifa, Volker Turk, ameeleza kusikitishwa na hatua hiyo.
Mbali ya Turk, Jumuhiya za kimataifa nazo zilipaza sauti kumtaka Rais Faye kutokusaini, jitihada ambazo hata hivyo hazijaweza kuzaa matunda.
Kwa mujibu wa Serikali, hatua hiyo imetokana na mtazamo wa raia wa Senegal juu ya vitendo vya mapenzi ya jinsia moja nchini humo.


