KAMPALA, Uganda
MKUU wa majeshi wa Uganda amesema wako tayari muda wowote kuisaidia Israel endapo itazidiwa nguvu katika vita dhidi ya Iran.
Hata hivyo, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter).
Jenerali Kainerugaba amedai kuwa matarajio yao ni kuona mataifa hayo (Israel na Iran) yanamaliza mgogoro huo wa Mashariki ya Kati.
“Tunataka kuona vita vya Mashariki ya Kati vikimalizika. Dunia imechoshwa na vita hivyo.
“Lakini, chochote kitakachofanyika kwa ajili ya kuharibu Israel, basi kitatuingiza vitani,” amesema.
Aidha, kauli yake hiyo inaendeleza matamko yake ya utata anayoendelea kuyatoa kiongozi huyo wa jeshi la Uganda.
Wiki chache zilizopita, Jenerali Kainerugaba alizua taharuki baada ya kusema Uganda ina mpango wa kumjengea sanamu Yonatan ‘Yoni’ Netanyahu.
Yoni, ambaye ni kaka wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliuawa akiwa komando wa jeshi la Israel katika vita ya Entebe, Uganda, mwaka 1976.


