JERUSALEM, Palestina
MIAKA miwili iliyopita, Sarah Qanan alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wakifanya vizuri darasani. Ndoto ya kuwa daktari ilikuwa kichwani kwake na kumuongezea morali ya kusoma kwa bidii.
Ikiwa imebaki miezi michache kufanya mtihani wake wa mwisho wa elimu ya sekondari, yaliibuka mapigano katika Ukanda wa Gaza mwishoni mwa mwaka 2023.
Kwamba mashambulizi ya vikosi vya wanajeshi wa Israel kwa Wapalestina yalichimba kaburi na kuzika ndoto kubwa za udaktari alizokuwa nazo Sarah.
Kwa sasa, Sarah mwenye umri wa miaka 18, anaishi kwenye hema akiwa na wazazi wake, moja ya familia nyingi zinazopitia maisha hayo ya mateso katika Ukanda wa Gaza.
Tofauti na miaka miwili iliyopita, ambapo ndoto zilikuwa ni udaktari, kwa sasa Sarah mwenye umri wa miaka 18 anasema kuishi ndiyo kipaumbele pekee kwake.

“Sisi wanafunzi tumeumizwa zaidi na vita hivi. Tumekuwa kwenye mateso haya kwa miaka miwili. Maisha yetu yamesimama kwa miaka miwili,” anasema Sarah na kuongeza: “Maisha yetu yaliyokuwa na ndoto nyingi nzuri yamebaki bure.”
Kwa upande mwingine, binti huyo ni miongoni mwa wanafunzi zaidi ya 650,000 waliokwama kuendelea na masomo huko Gaza, Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) linaeleza.
Baada ya vita kuanza, Oktoba, 2023, majengo ya shule ndiyo yaliyotumika kuwahifadhi watu waliopoteza makazi kutokana na nyumba zao kusambaratishwa na mabomu ya Israel.
Ni kwa mujibu wa UNICEF, asilimia zaidi ya 95 ya majengo ya shule katika Ukanda wa Gaza yaliharibiwa na mabomu ya Israel.
Kama hiyo haitoshi, ripoti ya UNICEF iliweka wazi kuwa mabomu ya Israel yalishambulia na kutekeleza vyuo vikuu vyote 12 vilivyokuwa katika Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia zaidi ya 87 ya majengo ya shule za Gaza yanahitaji marekebisho makubwa kuweza kutumika tena.
Baba yake Sarah, Ibrahim Qanan, anasema: “Kama familia, tulifanya kila linalowezekana kutimiza ndoto ya Sarah ya kusomea udaktari. Vita vimetuumiza, vimeyafanya maisha yetu kupinduka.”
Aidha, baba huyo wa watoto sita anaongeza: “Vita hivi vimekuwa vigumu sana kwa jamii ya Wapalestina, hasa kwa kitendo cha Israel kuharibu kwa makusudi vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu, zikiwamo shule za sekondari za Serikali na zile za awali.”
Ni kutokana na hali hiyo, wanafunzi takribani 40,000 walishindwa kufanya mtihani yao ya kuingia vyuo vikuu, hivyo kubaki wakiwa hawajui hatima yao katika safari ya elimu.
Kwa badhi ya familia, licha ya kuishi kwenye mahema kwa kukosa makazi, wazazi wameamua kubeba jukumu la kuwafundisha watoto wao, ingawa wanakiri kuwa bado kuna ugumu wanapitia.


