WASHINGTON DC, Marekani
VATICAN imeweka wazi kuwa haitakuwa sehemu ya Bodi ya Amani ya Rais Donald Trump, licha ya kukiri kupokea mwaliko.
Awali, Bodi hiyo ililenga kutafuta suluhu ya Ukanda wa Gaza, kabla ya Rais Trump kubadili mtazamo na kusema itasimamia migogoro yote duniani.
Ikumbukwe, mataifa 19 yameshasaini kuwa sehemu ya Bodi hiyo aliyoianzisha Rais Trump, ambaye ndiye Mwenyekiti wake.
Januari, 2026 Bodi hiyo ilipeleka ombi kwa Papa Leo XIV lakini mamlaka za Vatican zimesema kiongozi huyo hatoshiriki.
Ni kutokana na kile kinachoelezwa na Vatican kuwa hakubaliani na uwepo wa Bosi ya Amani, ikiamini migogoro ya dunia inapaswa kushughulikiwa na Umoja wa Mataifa (UN).
“Ni kwamba kwa ngazi ya kimataifa, UN ndiyo inayosimamia hii migogoro ya dunia,” imeeleza taarifa ya Vatican na kuongeza: “Hicho ndicho tunachojaribu kusisitiza.”
Ifahamike kuwa Papa Leo amekuwa mkosoaji mkubwa wa sera za Rais Trump tangu alipochaguliwa kuiongoza Vatican.


