Na mwandishi wetu, Gazetini
WAUMINI wa Dini ya Uislam duniani kote wanakaribia kuingia kwenye ibada ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Ni ibada ya siku 29 au 30 kila mwaka inayohusisha kujizuia kula, kunywa na matendo yaliyobeba tafsiri ya kwenda kinyume cha maamrisho ya Allah (s.w.).
Je, ni yapi mengine usiyoyajua kuhusu Mwezi Mtukufu wa Ramadhan? Makala haya yanakuchambulia.
Mosi, ni mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiislamu na ni nguzo ya nne katika Dini hiyo yenye waumini wengi duniani.
Pili, si tu Qur’an, Vitabu vingine vitatu vitakatifu (Tawrat, Injili na Zaburi) navyo vilishushwa wakati wa Ramadhan.
Tatu, funga ya Ramadhan iliamrishwa mwaka wa pili baada ya tukio la ‘Hijra’ (kuhama kwa Mtume Muhammad kutoka Makkah kwenda Madina).
Nne, ushindi wa Waislam dhidi ya washirikina wa Makkah (vita vya Badr) ulipatikana katika Mwezi huu.
Tano, wakati wa funga (kuanzia alfajiri hadi Magharibi), ni haramu hata kwa mke na mume kufanya tendo la ndoa.
Swaumu (Kufunga): Waislamu wenye afya na uwezo hujizuia kula, kunywa, na tendo la ndoa kuanzia alfajiri hadi magharibi.
Ukombozi wa Makkah (Fathu Makkah): Tukio hili la kihistoria ambapo Makkah ilitekwa bila umwagaji damu lilifanyika mwezi wa Ramadhani.
Sita, si lazima kufunga kwa wagonjwa, wanaosafiri (umbali mrefu), wazee, wajawazito, wanaonyonyesha na wanawake wenye hedhi, ingawa watalipa baada ya kumalizana changamoto hizo.
Saba, huenda wengi hawafahamu kuwa zipo baraka nyingi katika kitendo cha kula ‘daku’, kama alivyosema Mtume Muhammad (s.a.w.). “Hakika daku ni baraka amekupeni Allah, hivyo basi msiiache.”
Nane, katika Mwezi huu, Mtume (s.a.w.) aliiteka Makkah (bila umwagaji wa damu) na kuirejesha chini ya himaya ya Waislam.
Tisa, katika Mwezi wa Ramadhan (Tarehe 10), alifariki mke wa kwanza wa Mtume (s.a.w.), Bi. Khadija.
Kumi, mke wake mwingine, Bi. Aisha, ambaye anatajwa kuwa amehusika kwa asilimia kubwa ya masimulizi ya mafundisho ya Mtume (s.a.w.), naye alifariki kipindi cha Mwezi huu.


