11.2 C
New York

Zanzibar yavunja rekodi ya watalii wa kimataifa chini ya Dk. Mwinyi

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

ZANZIBAR imeshuhudia ongezeko kubwa na la kihistoria la watalii wa kimataifa katika kipindi cha miaka sita iliyopita, mafanikio yanayohusishwa moja kwa moja na uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambaye ameifanya sekta ya utalii kuwa mhimili mkuu wa maendeleo ya kiuchumi ya visiwa hivyo.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Januari 18, 2026, idadi ya watalii wa kimataifa wanaotembelea Zanzibar imeongezeka kwa kasi kubwa tangu mwaka 2020, hatua inayoonesha matokeo chanya ya sera, mikakati na mageuzi yaliyoanzishwa chini ya uongozi wa Dk. Mwinyi.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa mwaka 2020 Zanzibar ilipokea watalii wa kimataifa 260,644. Idadi hiyo iliongezeka hadi 394,185 mwaka 2021, kabla ya kupanda hadi 548,503 mwaka 2022. Mwelekeo huo chanya uliendelea mwaka 2023 ambapo watalii 638,498 waliitembelea Zanzibar, na kufikia 736,755 mwaka 2024.

Mwaka 2025 uliweka rekodi mpya baada ya Zanzibar kupokea jumla ya watalii wa kimataifa 910,682, idadi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya sekta ya utalii visiwani humo. Ongezeko hilo linaonesha wazi imani ya dunia kwa Zanzibar kama kituo salama, chenye vivutio vya kipekee na mazingira rafiki kwa watalii na wawekezaji.

Mafanikio haya yanatokana na uongozi wa Dk. Mwinyi uliolenga kuimarisha diplomasia ya utalii, kuvutia uwekezaji wa kimkakati, kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege, bandari na barabara, pamoja na kuimarisha usalama na utulivu. Hatua hizo zimechochea kuongezeka kwa safari za moja kwa moja kutoka masoko makuu ya utalii duniani na kuongeza muda wa kukaa kwa watalii.

Kuongezeka kwa idadi ya watalii kumekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar kwa kuongeza mapato ya Serikali, kuchochea biashara ndogondogo, na kupanua fursa za ajira hususan kwa vijana na wanawake katika sekta za malazi, usafirishaji, huduma za utalii na ujasiriamali.

Kutokana na mafanikio hayo, Zanzibar imeendelea kutambuliwa kimataifa kama moja ya maeneo bora ya utalii duniani, jambo linaloimarisha ushindani wake katika soko la utalii wa kimataifa na kuipa nafasi ya kujenga uchumi jumuishi na endelevu.

Kwa ujumla, ongezeko hili la kihistoria la watalii wa kimataifa linathibitisha dhamira thabiti ya Serikali ya Awamu ya Nane ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kuijenga Zanzibar yenye uchumi imara, shindani na unaotegemea sekta ya utalii kama injini kuu ya maendeleo ya Taifa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img