8.2 C
New York

Usiyoyajua kuhusu Siku ya Elimu Duniani

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

JANUARI 24 ya kila mwaka, Dunia huadhimisha Siku ya Elimu. Siku ambayo jamii hukumbushwa juu ya umuhimu wa elimu bora kwa maendeleo endelevu.

Kwamba elimu haipaswi kuwa mafanikio ya kitaaluma pekee, bali pia iwe msingi wa kuandaa raia anayewajibika kwa ajili ya kesho iliyo bora kwa jamii inayomzunguka.

Kupitia Mkutano Mkuu wake wa Desemba, 2018, UN ilipitisha na kutangaza rasmi kuwa Januari 24 ya kila mwaka itakuwa Siku ya Elimu Duniani. Hivyo, Januari 24, 2019, Dunia iliadhimisha kwa mara ya kwanza Siku ya Elimu.

Kwa Umoja wa Mataifa, elimu si tu ni haki ya msingi kwa kila binadamu, bali pia ni nyenzo muhimu na inayopaswa kubebwa na kila jamii katika kuyaendea maendeleo endelevu.

Kila inapofika Januari 24, Umoja wa Mataifa unataka jamii zijikague kwa kuangazia changamoto zinazozuia upatikanaji wa elimu, ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa kijinsia, hasa kwa watoto wa kike.

Aidha, kila Siku ya Elimu huambatana na kaulimbiu yake. Kwa mwaka 2026, kaulimbiu iliyobeba maadhimisho ni ‘Nguvu ya Vijana katika Elimu’.

Kaulimbiu hiyo inalenga kuonesha umuhimu na dhima ya vijana na wanafunzi katika kuweka mustakabali wa elimu katika jamii zao.

Msingi wa kaulimbiu hiyo unaitaja jamii kufahamu kuwa wanafunzi hawapaswi kubaki kuwa ni wasikilizaji, bali wanapaswa kushiriki kwa kutoa mawazo yatakayoleta matokeo chanya katika mfumo wa elimu.

Kwamba badala ya kuachwa nyuma, wanafunzi wanaweza kushiriki kwa kutoa maoni juu ya mbinu za ufundishaji na sera za elimu zinazotumika.

Licha ya Umoja wa Mataifa kuitaja elimu kuwa ni haki ya binadamu, pia una matamanio ya kuona ikiwa silaha ya kupunguza umasikini.

Ndoto ya Umoja wa Mataifa ni kuona kila jamii ikiwa na mfumo bora wa elimu utakaowasaidia wahitimu kuajiriwa au kutengeneza ajira ili kuboresha maisha yao, familia na jamii zinazowazunguka.

Kwa upande wake, Tume ya elimu na Sayansi ya Umoja wa Mataifa (UNESCO) inatambua nguzo nne zinazoitafsiri elimu bora.

Mosi, elimu inapaswa kutoa maarifa mapya. Pili, iambatane na vitendo. Tatu, imsaidie kuishi na jamii, ikiwamo kuheshimu wengine. Nne, elimu imuongezee thamani mwanafunzi, imsaidie kukua na kujiamini.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img