LONDON, Uingereza
IDADI ya majeruhi na miili ya waliopoteza maisha imeongezeka kwa kasi, hivyo baadhi ya hospitali kuzidiwa. Ni nchini Iran, ambako maandamano yameendelea kushika kasi.
Kwa siku kadhaa sasa, yamekuwapo maandamano makubwa ya raia wanaoipinga Serikali iliyoko madarani kutokana na changamoto mbalimbali, zikiwamo za ugumu wa maisha.
Katika moja ya hospitali, daktari ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa baadhi ya miili imefikishwa ikiwa na majeraha ya risasi vichwani.
Matukio ya raia kuuawa yameendelea licha ya onyo la Marekani kwa Serikali ya Iran. Rais Donald Trump alisema hatasita kutuma wanajeshi wake nchini humo.
Katika taarifa yake kwa Iran, Trump alisema Marekani iko bega kwa bega na waandamanaji kwa kuwa wanatekeleza haki yao ya kuiwajibisha Serikali.
Maandamano makubwa hayo yalianzia Mji Mkuu wa Tehran, kabla ya kusambaa na sasa yanaripotiwa kufika katika miji zaidi ya 100.
Kwa mujibu wa kile kinachoelezwa na BBC, mauaji hayo yamesababisha vifo vya raia 26, wakiwamo watoto sita, pia polisi 14 nao wakipoteza maisha.


