LONDON, Uingereza
HATIMAYE mshambuliaji wa Arsenal, Bukayo Saka, ameungana na Cesc Fabregas katika orodha ya wachezaji waliochangia mabao mengi ya timu hiyo kwenye historia ya Ligi Kuu ya England (EPL).
Katika mchezo wa jana Januari 3, 2025, dhidi ya Bournemouth, Saka alitokea benchi na kutoa ‘asisti’ moja kwa Rice aliyefunga mabao mawili. Bao jingine lilifungwa na Gabriel Magalhaes.
Kwa kufanya hivyo, sasa Saka anakuwa amehusika katika mabao 105 ya EPL, sawa na mkongwe wa timu hiyo, Fabregas.
Hata hivyo, bado Thierry Henry ndiye anayeongoza kwa kuchangia Arsenal jumla ya mabao 249, akifuatiwa na Dennis Bergkamp (181), Robin van Persie (135), Ian Wright (123) na Theo Walcott (108).
Ushindi dhidi ya Bournemouth uliifanya Arsenal kukaa kileleni mwa msimamo wa EPL kwa tofauti ya pointi saba, kabla ya Manchester City inayoshika nafasi ya pili kumenyana na Chelsea leo Januari 4, 2026.


