Na mwandishi wetu, Gazetini
KWA miaka zaidi ya 20, mfumo wa vyuo vikuu na vile vya kati kuendesha baadhi ya kozi kupitia mtandao (e-learning), hasa kwa wanafunzi wa mbali, umejizolea umaarufu mkubwa duniani kote.
Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 49 ya wanafunzi duniani wamehitimu ngazi mbalimbali za elimu ya juu kupitia ‘e-learng’. Idadi hiyo itaongezeka kwa asilimia 57 kufikia mwaka 2027.
Mvuto mkubwa wa mfumo huo wa masomo kupitia mtandao unatokana na urahisi wake, ukionekana kudhibiti changamoto ya umbali na muda.
Kwamba badala ya mwanafunzi kutumia umbali mrefu kukifuata chuoni, anaweza kutumia simu yake ya mkononi au kompyuta na kusoma akiwa nyumani.
Pia, mfumo huo ulioanzishwa mwaka 2000 umekuwa na tija kubwa kwa wafanyakazi wanaotaka kujiendeleza kielimu. Kwamba unamwezesha kusoma, huku akiendelea na kazi.
Faida kwa waajiri ni kwamba ufanisi wa mfanyakazi huimarika kwa asilimia 15 hadi 25 pindi anapokuwa akiendelea na masomo akiwa kazini.
Hata hivyo, kwa mwanafunzi/mfanyakazi anayesoma kupita mtandao kuna mambo anayopaswa kuzingatia ili kufanikiwa.
Kubwa ni jitihada ya kutosha. Tofauti na kwenda darasani, kusoma mtandaoni kunahitaji uwezo wa kujisimamia, nidhamu ya kiwango cha juu.
Pia, kuna ishu ya kujali muda. Kujua ni muda wa somo husika, kujisomea na kukamilisha kazi zilizoelekezwa na mhadhiri ili kuepuka kuchelewesha au kufanya kwa presha.
Licha ya changamoto hizo, kwa sasa bado masomo kupitia mtandao ni kimbilio la wanafunzi zaidi ya asilimia 70 duniani kote.


