MERSEYSIDE, Uingereza
BAADA ya suluhu dhidi ya Leeds United katika mchezo wa jana Januari Mosi, 2026, kocha wa Liverpool, Arne Slot, ameelekeza lawama zake kwa mwamuzi wa kati.
Mchezo huo wa Ligi Kuu ya England (EPL) ulimalizika kwa matokeo ya 0-0 lakini Slot anaamini mwamuzi Chris Kavanagh aliwaokoa Leeds kwa kuwapa faida ya faulo nyingi.
Pia, kocha huyo raia wa Uholanzi amesema Kavanagh alifumbia macho matukio mengi ya wapinzani wao kupoteza muda.
Wakati huo huo, Slot anaamini Liverpool ilinyimwa penalti kwa tukio la Hugo Ekitike kuchezewa rafu ndani ya boksi na Jaka Bijol, ingawa staa wake huyo hakuanguka.
“Kama angeanguka, ni wazi ilikuwa penalti lakini naelewa kwanini hakutaka kuanguka. Wakati mwingine, msimu huu tumenyimwa penalti nyingi kwa sababu tu wachezaji wetu hawakuanguka,” amesema.
Hata hivyo, Slot hajaacha kuwapongeza Leeds United akisema wachezaji wake wa safi ya ulinzi walifanya kazi nzuri katika mchezo huo.


