LONDON, Uingereza
KLABU ya Chelsea imetangaza rasmi kumfungashia virago kocha wake raia wa Italia, Enzo Maresca, ikielezwa kuwa chanzo ni uhusiano mbaya kati yake na baadhi ya mabosi wake.
Uamuzi wa kumtimua kocha umekuja zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya Chelsea kuifuata Manchester City.
Pia, Maresca ameoneshwa mlango wa kutokea ikiwa ni miezi michache tu imepita tangu alipoiongoza timu hiyo kutwaa mataji mawili.
Maresca amekuwa akitajwa kutoelewana na baadhi ya viongozi klabuni hapo tangu baada ya mechi yao ya Desemba 13, mwaka jana, dhidi ya Everton.
Baada ya mechi hiyo ya Ligi Kuu ya England, kocha huyo alifichua kuwa alikuwa na siku mbili ngumu, ikitafsiriwa kuwa aliwekwa kitimoto na viongozi.
Kuondoka kwake Stamford Bridge kunazidisha kasi ya taaifa zinazomuhusisha na kibarua cha kuinoa Manchester City endapo Pep Guardiola ataondoka.


