Na mwandishi wetu, Gazetini
NI kweli Tanzania kupitia timu yake ya soka ya taifa ‘Taifa Stars’ imeuanza vibaya msimu huu wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025). Kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Nigeria ‘Super Eagles’. Hayakuwa matokeo mazuri.

Hata hivyo, kwa kile kilichooneshwa na vijana wa Stars katika mchezo huo, ni wazi kuna hatua kubwa imepigwa katika soka la Tanzania.
Ulitazama mchezo huo wa Kundi C kwa dakika zote 90? Umeona nini kwa Stars? Binafsi, yapo mengi mazuri niliyoyaona kwa upande wa Stars. Mosi, haukuwa mchezo wa upande mmoja, labda kama wengi walivyotarajia. Kila upande ulikuwa na maswali magumu kwa mwenzake.
Licha ya ukubwa wa Super Eagles, wakati fulani walihitaji kutumia ‘akili ya ziada’ ili kujibu maswali ya Stars ndani ya uwanja. Haikuwa mechi rahisi kwao. Katika mechi kubwa ya hadhi ile, usingetarajia kuona Stars ikitengeneza nafasi za kufunga. Ilifanya hivyo na kama zingetumika kwa ufanisi, huenda matokeo yangekuja tofauti pia.
Pili, uwepo wa wachezaji wanaokipiga nje ya Tanzania una maana kubwa. Katika kikosi kilichoanza dhidi ya Super Eagles, wachezaji wengi (6) wanacheza nje ya nchi.
Hata bao pekee la Stars lilifungwa na Charles M’mombwa anayecheza soka la kulipwa nchini Malta, akitumia ‘asisti’ ya Novatus Miroshi anayekipiga Ligi Kuu ya Uturuki.
Unaweza pia kuona mchango mkubwa waliokuwa nao Mbwana Samatta, Simon Msuva na hata Kelvin John ‘Mbappe’, ambaye aliingia akitokea benchi.
Pasi na kubeza kazi kubwa iliyofanywa na Zuber Foba, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na wengine wanaocheza soka la ndani, ukweli ulio wazi ni kwamba uwepo wa ‘ladha’ ya Ulaya kutoka kwa akina Miroshi umeongeza ubora na utulivu kikosini.
Unaweza kuwauliza juu ya hilo Wanigeria, ambao katika mchezo dhidi ya Stars, kikosi chao cha kwanza kilikuwa na mchezaji mmoja tu anayecheza soka lake barani Afrika. Tatu, ilikuwa ni dhidi ya Super Eagles. Hakuna namna unaweza kuwalaumu wachezaji wala benchi la ufundi la Stars, zaidi ya kuwapongeza.
Stars walicheza dhidi ya timu la daraja la juu mno. Nigeria ambayo ni ya 38 katika viwango vya sasa vya ubora wa soka duniani, wakati Tanzania ni ya 112.
Eagles ambayo katika kikosi chake cha kwanza dhidi ya Stars, ni kipa pekee (Stanley Nwabal) ndiye mchezaji anayecheza soka ndani ya Afrika. Naye yupo Afrika Kusini, moja ya nchi zenye Ligi Kuu bora barani humu.
Haikuwa kucheza Ulaya tu, bali unaizungumzia Super Eagles ambayo kikosi chake cha kwanza dhidi ya Stars kilikuwa nyota wawili wenye tuzo ya Mchezaji Bora wa CAF, Victor Osimhen (2023) na Ademola Lookman (2024).
Ulitaka akina Bakari Nondo Mwamnyeto wafanye nini zaidi ya kile kilichotokea ndani ya uwanja? Kama ingewezekana, basi ingekuwa ni miujiza tu na si vinginevyo.
Pia, wakati Stars ikiwa haijawahi hata kushinda mechi moja ya AFCON, ilikutana na Nigeria ambayo imeshiriki mara kadhaa na hata kutwaa ubingwa wa michuano hiyo. Ni kweli lolote linaweza kutokea katika soka lakini ungetarajia maajabu yapi yaiokoe Stars mbele ya Super Eagles?
Hongera Taifa Stars, mapambano yanaendelea …


