LONDON, Uingereza
KICHAPO cha mabao 3-0 kutoka kwa Nottingham Forest kimeiacha Tottenham ikiwa na pointi 22 pekee katika mechi 16 za msimu huu wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Ni miaka 17 imepita tangu Tottenham ilipokuwa na idadi ndogo ya pointi kiasi hicho baada ya mechi 16 za mwanzoni mwa msimu.
Hivyo, ni wazi sasa kibarua cha kocha Thomas Frank kipo hatarini, kama ilivyokuwa kwa Juande Ramos katika msimu wa 2008-09.
Tottenham wamefungwa na Nottingham wakitokea kupata ushindi katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Brentford na Slavia Prague. Katika michezo hiyo, Tottenham ilikuwa kwenye kiwango bora, ikifunga mabao matano na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja pekee.
Dhidi ya Nottingham, mambo yalikuwa mabaya kwa Tottenham baada ya Callum Hudson-Odoi kufunga mabao mawili, kabla ya Ibrahim Sangare naye kuingia kambani. Ni kwa matokeo hayo, Tottenham sasa imepoteza mechi sita tangu msimu huu wa EPL ulipoanza kutimua vumbi Agosti, mwaka huu.


