Na mwandishi wetu, Gazetini
KUMEKUCHA! Droo ya hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia ilichezeshwa nchini Marekani.
Kwa mara ya kwanza, fainali hizo zitashirikisha mataifa 48, huku mechi 104 zikitarajiwa kuchezwa katika viwanja mbalimbali vya Marekani, Mexico na Canada.
Tukijikumbushe; timu 42 zilishakata tiketi na sasa zinasubiriwa zingine sita zitakazopatikana kupitia mechi za ‘play-off’ zitakazochezwa Machi, mwakani.
Sasa, makala haya yanaliangazia Kundi F na kuchambua timu zilizopo kuelekea michuano hiyo itakayoanza Juni 11, mwakani. Katika Kundi hili, zinakutana Uholanzi, Japan, Tunisia na mshindi wa ‘playoff’ kati ya Ukraine, Sweden, Poland na Albania.
Chini ya kocha mzawa, Ronald Koeman, Uholanzi ilifuzu bila kupoteza mchezo, huku Memphis Depay akifunga jumla ya mabao nane.
Uholanzi itatupa karata yake ya kwanza kwa kuivaa Japan, ambayo hii ni mara yao ya nane mfululizo kushiriki fainali za Kombe la Dunia.
Japan ambayo ilikuwa moto katika mechi za kufuzu, ikifungwa moja pekee kati ya 16 ilizoshuka dimbani, walifunga mabao 54 na kuruhusu matatu pekee.
Tunisia walihakikisha wanashiriki kwa mara ya tatu mfululizo fainali hizo baada ya kukusanya pointi 28 kati ya 30 wakati wa mechi za kufuzu.
Endapo Sweden ya kocha Graham Potter itafuzu kupitia ‘playoff’, basi itakuwa ni kumbukumbu nzuri ya mwaka 1974 kuiona mechi ya Kombe la Dunia kati yao na Uholanzi.


