LOS ANGELES, Marekani
BINGWA wa ngumi za uzito wa juu duniani, Oleksandr Usyk, amemtaja Deontay Wilder kuwa ndiye bondia anayetamani kuzichapa naye katika pambano lijalo. Usyk raia wa Ukraine, hajapanda ulingoni tangu Julai, mwaka huu, ambapo alimtandika Daniel Dubois wa Uingereza na kutwaa ubingwa wa dunia jijini London.
“Nataka kuendelea kupigana hapo mwakani. Nataka kupigana na Deontay Wilder. Nafikiri litakuwa pambano zuri,” alisema bondia huyo mwenye umri wa miaka 38.
Wilder, ambaye amewahi kuwa bingwa wa WBC, anapitia kipindi kigumu kwani amepoteza mapambano yote makubwa mawili tangu alipopigwa na Tyson Fury.
Staa huyo wa ngumi nchini Marekani, alipigwa na Joseph Parker mwaka 2023, kabla ya kutandikwa tena mwaka jana alipokutana na Zhilei Zhang.
Ni takribani mwaka mmoja umepita tangu bondia huyo mwenye umri wa miaka 40 alipomchapa kwa ‘KO’ ya raundi ya saba bondia asiye na jina, Tyrrell Anthony Herndon.


