Na mwandishi wetu, Gazetini
KUELEKEA Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu uliofanyika Jumapili ya wiki iliyopita, Rais Umaro Sissoco Embalo alishajiweka kwenye nafasi nzuri ya kushinda kutokana na kile kinachoendelea kwa wapinzani wake.
Embalo anawania muhula wake wa pili madarakani baada ya ushindi uliompeleka Ikuku katika Uchaguzi uliopita wa mwaka 2019.
Mwaka 2023, Rais huyo alivunja Bunge lililokuwa na wawakilishi wengi kutoka vyama vya upinzani baada ya kile alichokiita kuwa ni jaribio la kupindua Serikali yake katika machafuko yaliyojitokeza.
Lakini, kwa mtazamo wa wachambuzi wa siasa na wakosoaji wake, Rais Sissoco Embalo alifanya hivyo ili kupunguza nguvu ya upinzani.
Pia, wengi hawakubaliani na hatua yake ya kubaki madarakani baada ya kumaliza muhula wake. Mahakama ilimbakiza Ikulu hadi Septemba 4, kabla ya kusogeza tena Uchaguzi hadi Novemba.
“Ingawa muhula wake ulikwisha Februari, mwaka huu, alibaki madarakani kwa lengo la kukandamiza upinzani,” anasema mwandishi wa habari wa Guinea-Bissau, Bacar Camara.
Kwa sasa, siasa za upinzani nchini humo hazionekani kuwa na nguvu. Kati ya vyama 14 vinavyowania majimbo 102, ni kimoja pekee cha upinzani (No Kumpu Guine) kinachopewa nafasi ya kuvuna viti vingi katika Bunge lijalo.
Cha kushangaza, kwa mara ya kwanza katika historia ya Guinea-Bissau, Chama kilichopigania na kufanikisha uhuru wa nchi hiyo mwaka 1974, PAIGC, hakikushiriki Uchaguzi.
Kwanini? Ni Chama kinachoongozwa na Domingos Simoes Pereira, ambaye ndiye mpinzani mkubwa wa Rais wa sasa, Embalo.
Pereira aliondoshwa kwenye kinyang’anyiro cha urais Oktoba, mwaka huu, kwa kile kilichoelezwa na Mahakama Kuu kuwa alichelewa kurejesha fomu. Kwa wachambuzi, hizo zilikuwa ni siasa za kumzuia kushiriki Uchaguzi.
Wakati huo huo, mtaalamu wa masuala ya uhalifu, Lucia Bird, anasema hakukuwa na usawa wakati wa kampeni, ambapo wapinzani walikutana na vigingi vingi kutoka kwa vyombo vya usalama.
“Ni tofauti na ilivyokuwa kwa Embalo, ambaye alikuwa huru kuendesha mikutano yake ya kampeni, wakati wapinzani wakikutana na vizuizi vingi,” anasisitiza Bird.
Kwa sasa, tumaini pekee la upinzani katika kinyang’anyiro cha urais ni mgombea binafsi, Fernando Dias, ambaye anaungwa mkono na Waziri Mkuu wa zamani, Domingos Simoes Pereira. Ni tofauti na wengine, wakiwamo Jose Mario Vaz na Baciro Dja.
Katika hatua nyingine, hatari kubwa anayoiona Msemaji wa Taasisi ya Haki za Binadamu ya Guinea-Bissau, Guery Gomes Lopes, ni Uchaguzi wa mwaka huu kukosa uangalizi wa jumuhiya za kimataifa, zikiwamo Marekani, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya.
“Hii ni mara ya kwanza kuona hakuna jumuhiya za kimataifa katika Uchaguzi. Hatujui kama hazikualikwa au ziliamua kutokujihusisha,” anasema Lopez.
Mbaya zaidi, vyombo vya habari binafsi navyo vinapitia wakati ngumu, kama ambavyo mashirika ya utangazaji ya Ureno, RTP Africa na RDP Africa, yalivyozuiwa kufanya kazi tangu Agosti, mwaka huu.
Hata vyombo vya habari vya ndani vinavyoendelea kufanya kazi, bado vimekuwa vikibanwa, ikiwamo kulazimishwa kuripoti yale tu yanayosifia Serikali iliyoko madarakani.
Guinea-Bissau ni moja ya mataifa yanayokabiliwa na kiwango kikubwa cha umasikini, kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia (WB), pia ikisifika kwa usafirishaji wa dawa za kulevya.
Tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ureno miaka 50 iliyopita, nchi hiyo imekuwa na matukio kadhaa ya wanajeshi kupindua Serikali.
Published:


