LONDON, Uingereza
PSG wataikaribisha Bayern Munich katika nusu fainali ya kwanza msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, mchezo utakaochezwa kesho Aprili 28, 2026 mjini Paris, Ufaransa.
PSG walifika nusu fainali baada ya kuing’oa Liverpool kwa kichapo cha jumla ya mabao 4-0, wakati Bayern waliitoa Real Madrid kwa ushindi wa jumla ya mabao 6-4.
Katika soka la ndani, PSG wametoka kuifunga Angers mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu, hivyo wako kileleni mwa msimamo wa Ligue 1 kwa tofauti ya pointi sita.
Msimu huu, PSG ni mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa na wanaisaka rekodi ya kuwa timu pekee baada ya Madrid kuweza kulibeba misimu miwili mfululizo.
Bayern wao wametoka kuifunga Mainz 05 na tayari ni mabingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).
Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa, vigogo hao wa Bundesliga wanalisaka taji lao la kwanza tangu walipotwaa miaka sita iliyopita.
Rekodi inayoweza kuwapa jeuri ni ushindi wa mechi zote tatu zilizopita walizocheza ugenini dhidi ya PSG.
Kwa ujumla, PSG imeshinda mara sita pekee katika mechi 15 ilizokutana na Bayern hivi karibuni kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Vikosi: Bayern (4-2-3-1): Neuer, Kimmich, Upamecano, Tah, Stanisic, Pavlovic, Laimer, Diaz, Musiala, Olise, na Kane.
PSG (4-3-3): Safonov, Mendes, Pacho, Marquinhos, Hakimi, Neves, Beraldo, Zaire-Emery, Doue, Dembele, na Kvaratskhelia.


