LONDON, Uingereza
TANGU walipotwaa ubingwa mwaka 2006, timu ya taifa ya Italia haijavuka hatua ya makundi katika fainali za Kombe la Dunia.
Na badala yake, imeishia makundi mara mbili na kushindwa kufuzu fainali hizo mara zote mbili zilizopita (2018 na 2022).
Kwa sasa, kiungo wa zamani wa timu hiyo, Gennaro Gattuso, ambaye alikuwa kikosini mwaka 2006, ndiye kocha mkuu.
Gattuso amepewa mikoba, licha ya kwamba ana rekodi isiyovutia ya kufukuzwa na klabu 10 katika miaka 12 ya hivi karibuni.
Mtihani unaomsubiri kwa sasa ni kuiwezesha Italia kukata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu zitakazoanza Juni.
Aliiongoza timu yake hiyo kupata ushindi dhidi ya Ireland ya Kaskazini katika mchezo wa nusu fainali ya ‘play-off’ na sasa atakabiliana na mshindi kati ya Wales au Bosnia kugombea nafasi ya kwenda Kombe la Dunia.
Gattuso amepewa mikoba ya kocha mkongwe, Luciano Spalletti, ambaye alifungashiwa virago Juni, 2025.
Spalletti aliyeipa Napoli taji la Serie A alikuwa na kikosi cha Italia wakati kilipofika hatua ya 16 Bora ya Euro 2024.
Kama itakumbukwa, Spalletti alipewa kazi baada ya mkongwe mwingine, Roberto Mancini, kufukuzwa.
Kuondoka kwa Mancini kulikuja baada ya Italia kuwa mabingwa wa Euro, ingawa alishindwa kuiwezesha timu hiyo kufuzu Kombe la Dunia.
Kabla ya Gattuso kuajiriwa, zilikuwepo taarifa kuwa Claudio Ranieri ndiye aliyetakiwa kurithi mikoba ya Spalletti. Hata hivyo, kuajiriwa kwake kuinoa Italia kumekumbana na ukosolewaji wa baadhi ya wachambuzi wa soka nchini humo.
Kwa kuzitaja kwa uchache, Gattuso amezinoa Sion, Palermo, OFI, Pisa, Milan, Valencia, Marseille na Hajduk Split lakini hakuna aliyodumu nayo kwa miaka zaidi ya miwili.
Lakini, kipa wa zamani wa Italia, Gianluigi Buffon, ambaye naye ni sehemu ya wasaidizi wa Gattuso kwenye benchi la ufundi, ana mtazamo tofauti.
“Gattuso hana uzoefu mkubwa kuinoa timu aina ya Italia lakini wamemuajiri mtu mwenye morali ya ushindi.
“Nafikiri ndiyo maana amechaguliwa, ili kuleta fikira chanya ambayo alikuwa nayo akiwa na jezi za AC Milan na Italia,” amesema Buffon.
Tangu apewe mikoba, Gattuso ameshinda mara tano katika mechi sita, ingawa haikutosha kuiwezesha Italia kufuzu Kombe la Dunia, na badala yake inasubiri play off ili kujihakikishia tiketi.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wachambuzi pia wanasema tatizo si Gattuso, bali soka la Italia linaloonekana kupotea kwenye ramani.
Katika hilo, hoja yao ni kwamba soka la Italia halizalishi vikubwa kama zamani, na ndiyo maana hata klabu zake hazifanyi vizuri Ligi ya Mabingwa Ulaya na michuano mingine ya UEFA.
Ukiacha uwepo wa Buffon, pia Gattuso amemvuta kwenye benchi la ufundi mkongwe mwingine wa Italia, Leonardo Bonucci.
Je, kwa msaada huo wa Buffon na Bonucci, Gattuso aliyestaafu timu ya taifa akiwa amecheza mechi 73 ataipeleka Italia katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu?


