10 C
New York

Tanzania yaanza kuchukua hatua kukabili mabadiliko ya tabianchi

Published:

Belem, BRAZIL

Serikali ya Tanzania kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha wananchi hawakatizwi tena na mafuriko yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, kwa kujenga na kukarabati miundombinu muhimu kama madaraja na barabara katika maeneo yenye athari kubwa.

Akizungumza katika Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 30) unaofanyika Belem, Brazil, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI (Miundombinu), Mhandisi Rogatus Mativila alisema miradi inayoendelea imejikita katika kuokoa maisha na uchumi wa wananchi.

Kwa muda mrefu, wakulima, wafanyabiashara wadogo, wanafunzi na wagonjwa wamekuwa wakikwama kuvuka kutokana na barabara kukatika kila msimu wa mvua. “Mpango wa SCALE unaolenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya jamii kupitia fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia utasaidia kupunguza changamoto hizi kwa kuwa unawawezesha wananchi wenyewe kupanga na kutekeleza miradi ya kukabiliana na tabianchi,” alisema Mativila.

Kupitia mpango huo, ambao unatarajiwa kuwafikia watu zaidi ya milioni 6.6 katika mamlaka 65 za Serikali za Mitaa-54 Tanzania Bara na 11 Zanzibar_wananchi wataweza kupata miundombinu salama, hususan vijijini ambako athari za tabianchi zimekuwa zikiathiri uzalishaji na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Mhandisi Mativila alisema mpango huo umeweka msisitizo maalumu kwa makundi kama wanawake na vijana ambao mara nyingi ndio waathirika wakuu wa mafuriko na ukame, kwa kuwapa nafasi katika maamuzi na utekelezaji wa miradi ya mazingira.

Aidha, alitaja TARURA na DART kama taasisi muhimu zinazoendelea kujenga miundombinu imara ya usafiri na usafirishaji ambayo itasaidia sio tu kukabiliana na athari za tabianchi, bali pia kufungua fursa mpya za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa hatua hizi, wananchi wengi wanatarajia kuona maboresho makubwa katika maisha yao—kuanzia usalama wa watoto wanaokwenda shule, urahisi wa kusafirisha mazao, hadi kupungua kwa gharama zinazotokana na uharibifu wa miundombinu pindi mafuriko yanapotokea.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img