Na Mwandishi Wetu, Gazetini
MAKAMU wa Rais mstaafu wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, ametoa wito kwa Serikali kuongeza nguvu na mamlaka zaidi kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kulinda mazingira ya nchi dhidi ya uharibifu unaoongezeka kwa kasi.
Akizungumza Novemba 11, 2025, nyumbani kwake Mayamaya, Dodoma, baada ya kutembelewa na uongozi wa NEMC, Dk. Mpango alisema hali ya mazingira nchini inatia wasiwasi kutokana na uvamizi wa maeneo ya hifadhi, uchepushaji wa mito kinyume na taratibu, na uharibifu wa mabwawa ya kuzalisha umeme unaosababishwa na shughuli za kibinadamu.

“Biashara ya mbao na mkaa imeongeza kasi ya ukataji miti na kuchochea uharibifu wa misitu nchini. Ni muhimu NEMC kupewa nguvu zaidi katika utekelezaji wa sheria; sauti ya NEMC isiwe tena sauti ya mtu aliye nyikani,” alisema Dk. Mpango.
Aliongeza kuwa mifugo isiyo na utaratibu, uchimbaji holela wa mashamba na mimea vamizi ni changamoto zinazohitaji mikakati madhubuti ya kitaifa, huku akihimiza utekelezaji wa mpango wa Kijanisha Mazingira (Greening the Environment).
“Ni lazima tujiulize kama Taifa na kama miji, tumechukua hatua gani za kulinda na kurejesha uoto wa asili? Inawezekana kabisa kuwa na mazingira mazuri kama tutadhibiti shughuli zetu kwa kufuata sheria na mipango tuliyojiwekea,” alisisitiza.
Aidha, amependekeza kuanzishwa kwa green parks na botanical gardens katika majiji na miji mikuu ya nchi ili kujenga jamii rafiki kwa mazingira na yenye afya bora.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi, alimshukuru Dk. Mpango kwa maoni yake, akisema yatachangia kuimarisha juhudi za hifadhi endelevu ya mazingira nchini.
“Maono na ushauri wa Dk. Mpango ni dira muhimu kwetu katika kujenga Taifa lenye mazingira salama, safi na endelevu,” alisema Dk. Semesi.


