Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa wabunge sita katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa ya uteuzi wa wabunge hao imetolewa leo, Jumatatu Novemba 10, 2025 na ikisainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka.
Miongoni mwa walioteuliwa leo ni waliokuwa mawaziri, Dk Dorothy Gwajima (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum) na Balozi Mahmoud Thabit Kombo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Wengine ni aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na mbunge kwenye Bunge lililopita.
Dk Bashiru, Balozi Kombo na Dk Gwajima wameteuliwa kushika nafasi hizo kwa kipindi cha pili.
Uteuzi huo umemuhusisha pia Dk Rhimo Nyansako ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF). Yumo Abdullah Ali Mwinyi aliyekuwa Mbunge wa Mahond na Balozi Khamis Mussa Omar.


