8.8 C
New York

Dk. Judith Spendi: Uchumi na maendeleo yetu vimejengwa juu ya amani ya Tanzania

Published:

Mwandishi Wetu, Gazetini

ZIKIWA zimesalia siku chache kabla ya Watanzania kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, wito wa kudumisha amani na mshikamano umeendelea kutolewa kutoka kwa wadau mbalimbali, wakisisitiza umuhimu wa kulinda tunu hiyo adhimu ambayo imekuwa nguzo ya maendeleo ya taifa kwa miongo kadhaa.

Akizungumza leo Jumamosi, Oktoba 25, 2025, kutoka Cairo nchini Misri, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanamke na Nguvu ya Kijani, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Makampuni ya PMM 2001 Estate Ltd, Dk. Judith Spendi, amesema Watanzania wanapaswa kutambua kwamba amani ni urithi wa thamani ambao haupaswi kuchukuliwa kirahisi.

“Zaidi ya uchumi wa kampuni, tutunze amani yetu na tutunze mali Mungu aliyotupa kwa nguvu zote, kwa sababu watu wa nje hawawezi kuwa na nia njema na nchi yetu. Ndio maana mnasikia kelele zinatokea nje ya nchi, lakini sisi tusimame kama taifa moja lenye upendo na utulivu,” amesema Dk. Spendi.

Amani ni nguzo ya uchumi

Dk. Spendi ameeleza kuwa ukuaji wa biashara, uwekezaji na ustawi wa wananchi unategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa amani. Amesema kampuni nyingi za ndani na nje zimeendelea kufanya vizuri kutokana na mazingira mazuri ya kisiasa na kijamii ambayo Tanzania imejijengea kwa muda mrefu.

“Tanzania ni nchi ya amani, na hakuna sababu yoyote ya kufikiria kwamba amani itaondoka. Tusherehekee amani kama tunavyosherehekea mavuno, kwa sababu ndiyo msingi wa mafanikio ya sekta zote – kuanzia biashara, kilimo, elimu hadi afya,” amesisitiza.

Aidha, Dk. Spendi ameongeza kuwa falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ya 4R (Reconciliation, Resilience, Reforms na Rebuilding) imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha imani ya wawekezaji na wananchi katika Serikali, jambo lililosaidia kukuza uchumi na ustawi wa jamii.

“Sisi tunampenda Mama na tunapenda falsafa zake za 4R, kwa sababu ndizo zimefanya biashara zetu kukua. Hata huku nje, jina lake ni kubwa sana-watu wanazungumzia uongozi wake wa busara na namna alivyoleta heshima kwa Tanzania,” amesema Dk. Spendi.

Vijana wasiwe chanzo cha vurugu

Dk. Spendi pia ametoa wito maalum kwa vijana nchini kutumia nguvu zao katika kufanya kazi kwa bidii na kujenga taifa lenye misingi ya uadilifu. Amesema vijana wanapaswa kuwa walinzi wa amani na sio vyanzo vya vurugu, kwani wao ndio nguvu kazi na mustakabali wa taifa.

“Wito wangu kwa vijana ni tufanye kazi kwa bidii, tuwe waaminifu na watiifu kwa viongozi tuliowakabidhi usukani wa kutuongoza kutuongoza, ili sifa ya Tanzania isalie kuwa kisiwa cha amani. Vurugu havijengi, bali vinabomoa ndoto za wengi,” amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa jukumu la kulinda amani si la Serikali au vyombo vya ulinzi pekee, bali ni la kila Mtanzania popote alipo.

“Suala la kulinda amani si la polisi pekee, kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha tunabaki salama. Tunapoona dalili za uchochezi, tuwe wa kwanza kuzikemea. Huu ni wajibu wa kitaifa,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Dk. Spendi, viongozi wa dini wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri amani kwa vitendo kama ambavyo imeendelea kuhuhudiawa ili kuunganisha jamii.

 “Kulinda na kuishi kwa amani inapaswa kuwa kipaumbele. wawe watu wa kuhubiri amani kwa vitendo, maana ikitoweka kiongozi wa dini anachochea vurugu, huyo anakuwa amekiuka maadili ya kimungu,” amesisitiza.

Dk. Spendi ameeleza kuwa amani ni chanzo cha furaha ndani ya familia na jamii kwa ujumla, kwani inawawezesha watu kufanya shughuli zao kwa uhuru, watoto kupata elimu bora, na wafanyabiashara kufanya kazi zao bila hofu.

“Panapotokea vurugu, wanaodhurika zaidi ni wanawake, watoto na makundi maalum. Hawa ni watu wanaotegemea wengine ili wapate riziki. Tunapofikiria kuchochea vurugu, lazima tujiulize tuko tayari kuwaumiza watu hawa?” amehoji.

Amesema kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha kuwa nchi inaendelea kubaki salama, kwani nchi jirani ambazo zimekumbwa na migogoro zinaonyesha wazi thamani ya amani.

“Kwa mtu yeyote atakayejihusisha na vurugu, atakuwa amewakosea Watanzania, lakini pia amemkosea Mungu. Amani tuliyo nayo ni ndoto ya wengi katika mataifa jirani,” amesema kwa msisitizo.

Tanzania ya amani kwa maendeleo

Dk. Spendi ametoa wito kwa taasisi za kijamii, mashirika binafsi, wafanyabiashara na viongozi wa serikali kuendelea kushirikiana katika kuimarisha utamaduni wa majadiliano na kuheshimiana, hasa wakati huu wa uchaguzi.

Amesema Tanzania imejijengea heshima kubwa kimataifa kama “kisiwa cha amani,” na ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha jina hilo linaendelea kung’aa.

“Amani ni mali isiyo na bei. Tuitunze kwa vitendo, si kwa maneno. Kila mmoja wetu awe balozi wa amani mahali alipo,” amesema Dk. Spendi.

Kongamano la Amani

Kwa upande mwingine, Taasisi ya Mwanamke na Nguvu ya Kijani imeandaa Kongamano la Amani la Kitaifa, litakalofanyika kuanzia leo Oktoba 25 hadi 27, 2025 katika viwanja vya Posta, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Dk. Spendi, kongamano hilo litajumuisha viongozi wa dini, vijana, wanawake, wafanyabiashara na wadau wa maendeleo, likiwa na kaulimbiu: “Amani Kwanza, Uchaguzi wa Amani ni Uchaguzi wa Maendeleo.”

Lengo kuu la kongamano hilo ni kuhamasisha wananchi kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani, ikiwemo maandamano au lugha za chuki mitandaoni. Dk. Spendi amesisitiza kuwa wito huo unalenga kuwakumbusha Watanzania kuwa uchaguzi ni sehemu ya mchakato wa kidemokrasia, si vita.

“Kama tunavyokwenda kwenye nyumba za ibada kukumbushana amani, ndivyo tunavyopaswa kuishi nayo katika maisha ya kila siku. Bila amani hakuna kitu kitakachoendelea, maana amani na imani hukaa pamoja,” amesema.

Amehitimisha kwa kusema kwua Kongamano la Amani la Kitaifa linatarajiwa kuhitimishwa kwa tamasha la muziki na ngoma za asili litakalodumu kwa siku tatu, likiwa na lengo la kusherehekea amani kama sehemu ya mavuno ya taifa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img