6.4 C
New York

Polisi Dar yaonya vurugu wakati wa uchaguzi

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

IKIWA zimesalia siku chache kabla ya Tanzania kufanya uchaguzi mkuu, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, limetoa onyo kali kwa wale wote wanaopanga, kuratibu au kushiriki katika uvunjifu wa amani ikiwemo kufanya vurugu na maandamano siku ya Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi limekula kiapo cha kulinda nchi, raia na mali zao.

Akizungumza Ijumaa, Oktoba 24, 2025, wakati wa Kongamano la Vyuo na Vyuo Vikuu kuelekea Uchaguzi Mkuu lililofanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, Kamanda Jumanne Muliro, amesema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha usalama wa raia wote watakaoshiriki katika zoezi la kupiga kura.

“Tukiwa kama watu tuliokula kiapo, tunawaeleza kuwa tutatimiza jukumu letu la kuhakikisha watu wanakuwa salama. Wajitokeze kwa wingi kupiga kura, wafuate sheria, na sisi tutakuwepo barabarani kuwalinda wote wanaotekeleza jukumu lao la kikatiba. Siku hiyo kutakuwa hakuna maandamano wala vurugu – ni siku ya upigaji kura bila hofu,” amesema Muliro.

Kamanda huyo pia aliwataka vijana kuwa waangalifu na kutafakari kuhusu misukumo na mihemko yao, hasa kutokana na makundi au watu wanaoambatana nao, akisisitiza kuwa ni muhimu kudumisha amani.

Aliongeza kuwa kuwa na fikra chanya au hasi katika mijadala ya masuala ya kitaifa si kosa, lakini kugeuza mitazamo hiyo hasi kuwa vitendo vya vurugu ni kosa kisheria.

Muliro amehitimisha kwa kuwataka vijana kulinda hatma zao kwa kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kutawala nchini, ili waweze kufikia malengo yao ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

“Mtu ambaye hana vimelea vya uhalifu hawezi kuhofia akiona magari ya polisi. Atajisikia salama kuona ulinzi na amani vinaimarishwa, lakini wahalifu ndio watakao hofia. Sisi hatupo kwa ajili ya kutisha, bali kulinda watu na mali zao. Tarehe 29 Oktoba, 2025 ni siku ya kulinda haki ya kupiga kura, hivyo hakuna atakayeruhusiwa kuvuruga haki ya mtu mwingine. Tutawazuia na kuwakamata wote kwa mujibu wa sheria,” amesema Kamanda Muliro.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img