Na Mwandishi Wetu, Gazetini-Mwanza
Wakati dunia ikikabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira na afya unaosababishwa na moshi wa kuni na mkaa, Serikali imeendelea kusukuma mbele ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi kubwa za umma na binafsi.

Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, ameanza ziara ya kikazi mkoani Mwanza akiongozana na wataalam wa wizara hiyo, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa agizo la Serikali kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.
Ziara hiyo imeanza katika Manispaa ya Ilemela, ambako timu hiyo imetembelea shule tatu za sekondari zilizokwisha kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi kupitia Mradi wa CookFund, unaotekelezwa chini ya mpango wa kimataifa wa Integrated Approach to Sustainable Clean Cooking Solution, ukidhaminiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU).
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mlay alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) unaolenga kuhakikisha taasisi zote nchini zinatumia teknolojia rafiki kwa mazingira na afya.
“Tunataka kuona shule, hospitali, magereza na taasisi nyingine zikihama kutoka kwenye matumizi ya kuni na mkaa. Hii si tu inalinda afya za wapishi na wanafunzi, bali pia inalinda misitu yetu na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa,” amesema Mlay.

Ameongeza kuwa, walezi na walimu wanapaswa kuwa mabalozi wa elimu ya nishati safi ili wanafunzi nao wawe chachu ya mabadiliko katika jamii.
“Watoto hawa wakielimishwa mapema, watakuwa mabalozi wa nishati safi majumbani mwao,” ameisistiza.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Maalum wa Manispaa ya Ilemela, aliyemwakilisha Afisa Elimu Sekondari, amepongeza juhudi hizo na kusema kuwa tayari shule kumi ziko katika mpango wa matumizi ya nishati safi, hatua ambayo imeleta mabadiliko makubwa kwenye mazingira ya shule.
Walimu Wakuu wa shule zilizotembelewa-Bwiru Boys, Bwiru Girls na Buswelu Sekondari-walisema matumizi ya nishati safi yamepunguza gharama za uendeshaji, kuokoa muda wa upishi, na kuboresha usalama wa wapishi.
Timu hiyo ya wataalam pia ilitembelea shule ambazo bado zinatumia kuni na mkaa, ikizihimiza kuboresha mifumo yao na kuanza safari ya kutumia nishati safi ya kupikia kwa ustawi wa mazingira na afya za wananchi.


