9.5 C
New York

Ripoti: Uwindaji haramu wapungua, lakini faru bado wapo hatarini

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

TANZANIA imeendelea kuungana na nchi nyingine duniani katika kusherehekea Siku ya Faru Duniani kia ifikapo Septemba 22, huku takwimu mpya zikionyesha kuwa uwindaji haramu wa faru barani Afrika umeshuka hadi kiwango cha chini zaidi kwa miaka 11, lakini wataalamu wa ikolojia wanasema ukuaji wa idadi ya faru bado uko hatarini.

Kulingana na ripoti ya State of the Rhino 2025 ya International Rhino Foundation, faru mmoja aliuwawa kila masaa 15 barani Afrika mwaka jana. Hata hivyo, idadi ya faru kwa ujumla inaanza kurejea, huku idadi ya faru barani Afrika na Asia ikiongezeka kwa 430 tangu mwaka 2022, ikileta jumla ya faru duniani kufikia 26,700.

“Barani Afrika bado ndiko nyumbani kwa faru wengi zaidi duniani, ikiwemo faru mweusi aliye hatarini sana (black rhino) wenye takriban 6,788 na faru mweupe aliye karibu hatarini (white rhino) wenye idadi ya takriban 15,752,” inachambua ripoti hiyo.

Licha ya maendeleo haya, uwindaji haramu na biashara haramu ya pembe za faru bado vinaendelea kupunguza idadi ya faru, huku mahitaji makubwa yakiibuliwa na nchi za Vietnam na China. Pembe za faru hutumika katika tiba za kienyeji, mapambo na vitu vya kifahari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wild’s Africa, Peter Knights, amesema ingawa uwindaji haramu wa faru umepungua mwaka huu na idadi ya faru inakua, faru bado wapo hatarini kutokana na uwindaji wa pembe zao. Aliongeza kuwa uchunguzi wa uadilifu kwa walenzi umethibitishwa kuwa na ufanisi na unapaswa kutumika kwa wingi, sambamba na kampeni za elimu na kupunguza mahitaji katika Vietnam na China.

“Tangu kuanza kwa mgogoro wa uwindaji haramu mwaka 2008, faru zaidi ya 12,000 waliuawa haramu barani Afrika. Kiwango cha juu kilikuwa mwaka 2015, ambapo faru 1,349 waliuawa, ikilinganishwa na matukio 516 yaliyorekodiwa mwaka 2024, kiwango cha chini zaidi kwa zaidi ya muongo mmoja,” anasema Knights.

Ripoti ya African and Asian Rhinoceroses Status, Conservation and Trade iliyotolewa na CITES mwaka 2025, inaonyesha uwindaji ulisababisha hasara ya 2.15% tu ya idadi ya faru barani Afrika mwaka 2024, kiwango cha chini zaidi kwa miaka 13.

Mbinu za uhifadhi barani Afrika sasa zinajumuisha ulinzi shambani, ukaguzi wa kiintelijensia, ufuatiliaji kwa ndege, mafunzo ya kisasa kwa walenzi, ushirikiano na jamii za wenyeji, na uhamishaji wa faru kwenda maeneo salama.

Knights anasisitiza kuwa ingawa mafanikio ya hivi karibuni ni ya kuahidi, bado ni dhaifu. Mashirika yanapaswa kuendelea kuwekeza katika juhudi za kupambana na uwindaji haramu, kushirikiana kimataifa, na elimu kwa walaji kupunguza mahitaji ya pembe za faru duniani. Serikali, wahifadhi wanyamapori na wananchi wanahimizwa kuendelea kuwa makini, kulinda makazi ya faru, na kuripoti uhalifu dhidi ya wanyamapori.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img