6.4 C
New York

Kanisa la Anglikana lavunja mwiko wa miaka 500

Published:

London, UINGEREZA

KWA mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake takribani miaka 500 iliyopita, Kanisa la Anglikana limeandika historia mpya baada ya kumteua, Dame Sarah Mullally (63) kuwa Askofu Mkuu Mteule wa Canterbury.

Mullally, ambaye ana historia ya kipekee kitaaluma, kabla ya kujiunga na huduma ya kipadre, alijipatia umaarufu mkubwa katika sekta ya afya. Mwaka 1999 aliweka rekodi kwa kuteuliwa kuwa Afisa Mkuu wa Uuguzi akiwa na umri mdogo zaidi katika historia ya Uingereza. Hatua hiyo ilimjengea msingi imara wa uongozi na heshima ya kijamii kabla ya kuhamia kwenye maisha ya kiroho.

Kwa zaidi ya miaka saba iliyopita, amehudumu kama Askofu wa London, nafasi ambayo inamweka kwenye nafasi ya tatu kwa ukubwa miongoni mwa viongozi wa Kanisa hilo, huku pia akiwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo. Hatua hiyo ilionekana kama ishara ya mabadiliko makubwa katika taasisi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikumbwa na mijadala kuhusu nafasi ya wanawake katika uongozi wa kidini.

Wanawake waliruhusiwa kuwa mapadri katika Kanisa la Anglikana kuanzia katikati ya miaka ya 1990 pekee. Hata hivyo, bado kuna viongozi wa juu, wakiwemo baadhi ya maaskofu wakuu, wanaopinga vikali wanawake kushika nafasi za uongozi, wakiamini kwamba jukumu la kiroho linapaswa kubaki kwa wanaume pekee.

Kwa mujibu wa kanuni za Kanisa hilo, Maaskofu Wakuu wa Canterbury hulazimika kustaafu wanapofikisha umri wa miaka 70. Wapo waliodhani kuwa kizuizi hicho cha kisheria kingezuia Mullally kuteuliwa, lakini uteuzi wake umedhihirisha mwelekeo mpya na wa kihistoria.

Ingawa tarehe rasmi ya kutawazwa kwake haijatangazwa, tayari uteuzi huu umetajwa kuwa hatua kubwa ya mabadiliko, si tu kwa Kanisa la Anglikana, bali pia kwa mustakabali wa nafasi ya wanawake katika taasisi za dini duniani.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img