Na Hassan Mwasha, Gazetini
MIKUTANO ya kampeni inaendelea kote nchini. NI takribani mwezi mmoja tu umebaki kabla ya Watanzania kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Kupitia mchakato huo wa kidemokrasia, Watanzania watatumia boksi la kura kuchagua viongozi wao katika nafasi za rais, wabunge na madiwani, kama ambavyo hufanya kila baada ya miaka mitano kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Je, kuelekea siku hiyo, Watanzania wamepatiwa elimu ya kutosha juu ya thamani ya boksi la kura na uhusiano wake katika ustawi wa maisha yao, jamii na Taifa kwa ujumla?
Bado nashawishika kujiuliza; mamlaka zimewekeza jitihada za kutosha katika kuwafanya wananchi wafahamu namna boksi la kura lilivyo na umuhimu mkubwa kwao kwa kipindi cha miaka mitano ijayo?
Labda niliweke sawa, kwamba katika nafasi zote hizo, hata kama kiongozi atakuwa hafai, wananchi hawatakuwa na nguvu ya kumtoa madarakani hadi atakapomaliza miaka mitano.
Sasa, nikiwa sehemu ya wananchi, nimebahatika kuhudhuria baadhi ya mikutano ya kampeni na kuona mambo yanavyoendelea.
Ni katika mikutano hayo, ikiwamo inayoendelea katika makazi yangu wilayani Sumbawanga, Rukwa, nimesikitika kuona bado wapo wananchi wanaoichukulia siasa katika sura ya ‘ushabiki’ wa soka, ndondi au michezo mingine.
Kwa mikutano kadhaa niliyohudhuria na mingine kuifutailia kupitia vyombo vya habari, nimeona na kusikitishwa na jambo moja. Ni lipi hilo? Nitajaribu kueleza, nikiamiamini itafungua mjadala mpana wa namna wananchi wanavvyopa umuhimu mdogo boksi la kura katika kuamua maisha yao.
Katika mikutano hiyo, nimeweza kushuhudia mwendelezo wa namna baadhi ya wananchi wanavyoamua kujivisha ushabiki wa vyama vyao.
Kwamba kwao sera za mgombea au chama siyo kipaumbele kilichowapeleka katika mkutano. Na badala yake, wao wamejipanga kushangilia, kupiga vigelegele kwa kila watachokisikia kutoka kwa mgombea anayenadi sera zake jukwaani.
Pasi na nia ya kuwatusi, wao ni bendera inayofuata uelekeo wa upepo tu. Kwa lugha nyingine rahisi, pia unaweza kusema wamejitoa katika nafasi ya mwananchi anayepaswa kwenda kwenye mkutano wa kampeni kwa lengo la kusikiliza, kupima na hata kuhoji sera anazokuja nazo mgombea.
Ukijaribu kumfuatilia, utabaini kuwa asilimia kubwa ya wananchi wa aina hiyo wanatokea katika maisha yasiyo na uhakika wa milo mitatu, achilia mbali huduma bora za kijamii.
Kwa upande mwingine, ukifuatilia zaidi, unaweza kubaini kuwa katika mazingira wanayotokea, kuna changamoto nyingi ambazo wangehitaji kuwa na maswali magumu kwa wagombea ili kujua ni namna gani zingeweza kupatiwa ufumbuzi.
Wengine, katika maeneo yao, wagombea wanaoomba ridhaa mwaka huu walishindwa kumaliza kero nyingi baada ya kuchaguliwa katika Uchaguzi uliopita. Safari hii, wako jukwaani wakiomba kuaminiwa tena.
Lakini, kutokana na wananchi kuvaa ushabiki wa kushangilia, huoni wakiwauliza wagombea hao maswali magumu juu ya kile wanachoomba tena baada ya kushindwa kufanikisha katika awamu iliyopita.
Kinyume chake, wananchi wa aina hii wanakwenda kwenye mikutano ya kampeni wakiwa upande wa wagombea na lengo la kulinda hadhi ya vyama vyao. Wanakwenda wakiwa na sura zilizotamalaki ushabiki katika masuala ya msingi yaliyobeba hatima ya maisha yao na vizazi vyao.
Sasa tujiulize; endapo wananchi wenye sura hiyo wataendelea kupamba mikutano ya kampeni, tunaweza kuamini na kuitafsiri siasa kuwa ni silaha ya maendeleo kwa jamii na Taifa letu?
Published:


